WASHINGTON, AMERIKA
RAIS wa Amerika Donald Trump amelitaka kundi la Hamas liwaachilie mateka wote kufikia saa sita mchana Jumamosi, la sivyo atafuta makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na Hamas kisha mbingu zipasuke.
Katika kile kinachoweza kufasiriwa kuwa ‘atafyeka’ Hamas, Rais Trump amesema hatakubali Israel itatize juhudi zake kuhusu suala hilo na atashauriana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amwache apambane na kundi hilo la kipalestina.
Kiongozi huyo alisikitika kuwa masharti ambayo yaliwekwa na Hamas kabla ya kuwaachilia mkumbo wa mwisho wa mateka, hayavumiliki. Pia alikashifu vikali tangazo la kundi hilo kuwa wamesitisha kuwaachilia mateka zaidi wa Israel.
“Jinsi ninavyojua, iwapo mateka hao hawatawaachiliwa kufikia Jumamosi 12, nafikiri huo ni muda mzuri. Nitasema mkataba ufutwe, kila kitu kitu kichukue mkondo wake na mbingu zipasuke. Narudia tena lazima waachiliwe kufikia Jumamosi saa sita,” akasema Rais Trump.
Alisisitiza kuwa mateka hao lazima waachiliwe wote mara moja badala ya mtindo ambao umekuwa ukiendelea ambapo wanaachiliwa kwa mkumbo.
Rais Trump pia alionya kuwa atasitisha msaada kwa Jordan na Misri iwapo hawatawachukua Wapalestina ambao anapanga kuwaondoa ukanda wa Gaza.
Alikuwa akitarajiwa kukutana na Mfalme wa Jordan Abdullah mnamo Jumanne.
Pia rais huyo amesema kuwa Wapalestina hawatarejea Gaza baada ya Amerika kustawisha ukanda huo. Baadhi ya maafisa wa serikali yake wamekuwa wakisema Wapalestina watarejea ukanda huo baada ya ujenzi wake upya kukamilika.
Hata hivyo, Rais Trump amesema alifikiria angeingia makubaliano na Misri na Jordan kuwapokea Wapalestina akisema Amerika hutoa mabilioni ya dola kwa nchi hizo mbili kila mwaka.
Alipoulizwa iwapo Wapalestina watakuwa na haki ya kurejea Gaza, Trump alisema watakuwa na maisha bora na makazi mazuri Jordan na Misri kwa misaada ya Amerika.
“Nazungumzia kuwajenga makazi ya kudumu kwao. Watakuwa na nyumba nzuri na maisha ya kheri. Gaza itachukua miaka mingi ili ujenzi wake kukamilishwa kwa hivyo, Wapalestina hawatarudi,” akasema Rais Trump.
Mnamo Februari 2 baada ya kukutana na Netanyahu jijini Washington, Rais Trump alipendekeza kujengwa upya kwa Gaza ambapo alipendekeza raia wake milioni 2.2 waondolewe. Alisema Amerika inalenga kubadilisha ukanda huo kuwa ‘Nuru na Mwanga wa Mashariki ya Kati’
Wenyeji wa Gaza wamekataa pendekezo la Rais Trump huku wakiungwa mkono na mataifa ya Kiarabu, makundi ya kupigania haki na Umoja wa Kitaifa (UN).
Mmoja wa viongozi wa Hamas Sami Abu Zuhri alisema kauli ya Rais Trump kuwa Wapalestina hawatarejea Gaza inaonyesha chuki dhidi yao na tamaa yake ya kutwaa ardhi yao.
“Tunamwonya kuwa afahamu matamshi yake yanaweza kuzua vita Gaza,” akasema Zuhri huku akiapa Wapalestina hawataenda popote na kuiachia Amerika ardhi yao.
Leave a Reply