Trump ataka Mahakama ya Juu ya Amerika kuokoa TikTok nchini humo – Taifa Leo


RAIS mteule wa Amerika Donald Trump ameitaka Mahakama ya Juu ya nchi hiyo kusitisha utekelezaji wa sheria ambayo itapiga marufuku apu maarufu ya mtandao wa kijamii ya TikTok au kuilazimisha kuuzwa, akisema anapaswa kuwa na muda baada ya kuchukua madaraka ili kusaka “ utatuzi wa kisiasa” kwa suala hilo.

Mahakama itasikiliza kesi hiyo Januari 10.

Sheria inamtaka mmiliki wa TikTok kutoka China, ByteDance, kuuza jukwaa hilo kwa kampuni ya Amerika au ipigwe marufuku. Bunge la Amerika llilipiga kura Aprili kuipiga marufuku iwapo ByteDance hataiuza kufikia Januari 19.

TikTok, ambayo ina watumiaji zaidi ya milioni 170 nchini Amerika, imetaka sheria hiyo kufutwa. Lakini ikiwa mahakama haitotoa uamuzi unaoiunga mkono, apu inaweza kupigwa marufuku nchini Amerika Januari 19, siku moja kabla ya Trump kutwaa madaraka.

Usaidizi wa Trump kwa TikTok ni mabadiliko kutoka 2020, wakati alijaribu kuzuia apu hiyo nchini Amerika na kulazimisha uuzaji wake kwa kampuni za Amerika kwa sababu inatoka China.

Inaonyesha pia juhudi kubwa ya kampuni hiyo kutangamana na Trump na timu yake wakati wa kampeni ya urais.

“Rais Trump hachukui msimamo wowote kuhusu msingi wa mzozo huu,” alisema D. John Sauer, wakili wa Trump ambaye pia ndiye mteule wa rais wa wakili mkuu wa Amerika.

“Badala yake, anaomba kwa heshima kwamba Mahakama ifikirie kusitisha tarehe ya mwisho ya Januari 19, 2025, wakati inazingatia uhalali wa kesi hii, na hivyo kupatia utawala unaokuja wa Rais Trump fursa ya kutekeleza azimio la kisiasa la kesi hiyo,” aliongeza.

Trump hapo awali alikutana na Mkurugenzi Mtendaji wa TikTok,Shou Zi Chew mnamo Desemba, saa chache baada ya rais mteule kueleza alipendelea kuruhusu TikTok kuendelea kufanya kazi nchini Amerika angalau kwa muda kidogo.

Rais mteule pia alisema alipokea mabilioni ya maoni kwenye mtandao huo wa kijamii wakati wa kampeni yake ya urais.

TikTok haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*