RAIS wa Amerika, Donald Trump, ametangaza kuwa serikali yake itazima aina zote za ufadhili kwa Afrika Kusini kupinga sheria dhalimu ya ardhi inayotekelezwa na serikali ya nchi hiyo.
“Afrika Kusini inanyakua ardhi za watu wa matabaka fulani na kuwadhulumu vibaya,” Trump aliandika katika mtandao wa kijamii wa TruthSocial.
“Huu ni ukiukaji wa haki za kibinadamu na unafanyika wazi wakati kila mtu anaona,” Rais huyo akaongeza.
Trump alikuwa akirejelea sheria iliyotiwa saini juzi na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, inayolenga kuleta mageuzi katika sekta ya ardhi “kulinda masilahi ya umma” na kuondoa maovu ya tangu utawala wa ubaguzi wa rangi.
Amerika inabakia mshirika mkubwa kwa kisiasa na kiuchumi kwetu sisi Afrika Kusini. Lakini usipohesabu msaada wa PEPFAR ambao unachangia kwa asilimia 17 mradi wa kukabiliana na Ukimwi nchini mwetu, hakuna msaada wowote mwingine ambao Afrika Kusini inapokea kutoka kwa Amerika
“Hatua hii ni kielelezo cha kujitolea kwa chama cha ANC kuondoa unyakuzi wa ardhi wa nyakati za ukoloni na kuhakikisha kuwa ardhi na rasilimali nchini Afrika Kusini zinatumika kwa manufaa ya wananchi wengi,” chama hicho tawala kikasema baada ya Rais Ramaphosa kutia saini sheria hiyo.
Wakosoaji wanasema sheria hiyo ni dhalimu, haswa kwa sababu inairuhusu serikali kutwaa ardhi kutoka kwa watu fulani hata bila kuwalipa fidia.
Kwa upande wake, Rais Trump alisema: “Amerika haitakubali sheria hii, tutachukua hatua. Vilevile, nitaondoa aina zote za ufadhili kwa serikali ya Afrika Kusini hadi uchunguzi wa kina kuhusu hali hii utakapokamilika!”
Lakini akijibu tangazo hilo kupitia akaunti yake ya X (zamani Twitter), Rais Ramaphosa alikanusha kwamba serikali yake inatwaa ardhi visivyo akisema kinachofanyika ni kugeuza matumizi ya ardhi ya umma ili kufaa wale ambao wamebaguliwa kwa muda mrefu.
Kuhusu kupokea ufadhili ambao sasa Trump amesema amesitisha, Ramaphosa alikuwa na haya ya kusema:
“Amerika inabakia mshirika mkubwa kwa kisiasa na kiuchumi kwetu sisi Afrika Kusini. Lakini usipohesabu msaada wa PEPFAR ambao unachangia kwa asilimia 17 mradi wa kukabiliana na HIV nchini mwetu, hakuna msaada wowote mwingine ambao unapokewa na Afrika Kusini kutoka kwa Amerika,” akahitimisha.
Bwanyenye Elon Musk, ambaye ni mshirika wa karibu wa Trump na mmoja wa maafisa wakuu katika utawala wa sasa, alizaliwa nchini Afrika Kusini mnamo 1971 wakati wa enzi za utawala wa ubaguzi wa rangi. Alipata uraia wa Amerika mnamo 2022.
Akiongea juzi katika Mkutano wa Ulimwengu kuhusu Uchumi jijini Davos, Uswisi, Rais Ramaphosa alisema anatarajia kufanya kazi kwa ushirikiano mzuri na Rais Trump.
“Nilizungumza naye baada ya ushindi wake na kumpongeza. Tulikubaliana kuwa tutakuwa tukifanyaka kazi pamoja,” akasema.
Leave a Reply