Tutamzima Ruto dhidi ya kuingiza wapiga kura kutoka nchi jirani – Taifa Leo


KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka amedai serikali inapanga njama ya kusajili raia wa kigeni kuwa wapiga kura nchini ili kama njia ya kuendeleza udanganyifu katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Bw Musyoka alidai, bila ithibati yoyote, kwamba kuondolewa kwa hitaji la kupigwa msasa kwa watu kutoka eneo la Kaskazini Mashariki kabla ya wao kupewa vitambulisho vya kitaifa ni sehemu ya njama ya kuingiza wapiga kura kutoka taifa jirani la Somalia.

Makamu huyo wa rais wa zamani alisema kuwa hatua iliyotangazwa na Rais William Ruto wakati ziara yake eneo limechochewa kisiasa kwa manufaa yake katika uchaguzi mkuu ujao.

Bw Musyoka alidai Rais amepoteza umaarufu sehemu zote za nchi na ameamua kutumia mbinu za kuhatarisha usalama wa kitaifa ili kusalia mamlakani 2027.

“Serikali zote zilizopita hazikukosea kwa kusisitiza kuwa sharti wanaotuma maombi ya vitambulisho wapigwe msasa kubaini ikiwa wao na raia halisi wa Kenya. Kuondolewa kwa hitaji hilo lina athari za kiusalama nchini na kimataifa,” akaeleza.

Bw Musyoka alisema hatua hiyo ya kuingiza wageni nchini na wakuwasajili kuwa wapiga kura itafeli kwa sababu Wakenya wako macho na watahakikisha kuwa kura haziibiwi 2027.

Kiongozi huyo wa Wiper alitaja uchaguzi wa hivi majuzi nchini Ghana ambapo chama tawala cha New Patriotic Party (NPP) kilikabiliwa na tuhuma za kuingiza wapiga kura kutoka nchi jirani ya Burkina Faso. Hata hivyo, chama hicho bado kilishindwa na chama cha upinzani cha National Democratic Congress katika uchaguzi huo ulifanyika Desemba mwaka jana.

“Rais wa Ghana walikuwa macho zaidi kiasi cha kuwaonya wapiga kura walioletwa kutoka nje kwamba wangeteketezwa endapo wangethubutu kupiga kura nchini humo. Onyo hilo lilizima kabisa mipango hiyo ya wizi wa kura,” akasema.

Bw Kalonzo alisema hayo wakati wa hafla ya mazishi ya aliyekuwa msaidizi wake Daniel Kimanzi Maunga katika eneo la Tiva, eneo bunge la Kitui ya Mashambani, Kaunti ya Kitui.

Bw Musyoka alisema kuzomewa kwa Rais Ruto mjini Isiolo Ijumaa kulikuwa kielelezo cha Wakenya kukosa imani na utawala wa Kenya Kwanza.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*