Tutasimama na Kanisa linalolaaniwa kwa kusema ukweli-Kalonzo – Taifa Leo


 

KIONGOZI wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ameikashifu Serikali ya Kenya Kwanza kwa kulaani msimamo wa kanisa katoliki kuhusu michango ya kutiliwa shaka kutoka kwa wanasiasa.

Kalonzo, ambaye aliandamana na mwenzake wa Democratic Action Party-Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa, alizungumza katika Kanisa la St Joseph the Worker Parish katika Racecourse, Nakuru City, wakati wa Misa ya Jumapili.

Makamu huyo wa rais wa zamani alisema kuwa Kanisa Katoliki limetoa mwelekeo wa jinsi nchi inavyopaswa kutawaliwa kwa kuzingatia Utawala wa Sheria na kwa kumcha Mungu.

“Kanisa limeweka msimamo kuhusu jinsi nchi inapaswa kuongozwa kwa mujibu wa Katiba ya Kenya na hivyo ndivyo tunavyopaswa kufuata. Rais Ruto anapaswa kusikiliza kwa makini kanisa, kwa sababu huyo ni Mungu anayezungumza kupitia watu wake waliowekwa wakfu,” alisema Bw Musyoka.

Viongozi wengine walioandamana naye ni pamoja na aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, Seneta Wambua(Kitui) na madiwani kadhaa.

Huku akibainisha kuwa mamlaka ya kanisa ni muhimu, Bw Musyoka alisema licha ya Maaskofu kuchukua msimamo viongozi wa Kenya Kwanza wameendelea kuwaalani badala ya kuheshimu mwongozo uliotolewa.

“Ninaomba kanisa lituombee ili tuwe na ujasiri kama Maaskofu wa Kikatoliki, kwa kuwa na msimamo na kukataa siasa za migawanyiko, uwongo, ufisadi na ambazo zimegawanya nchi yetu,” aliongeza Musyoka.

Kalonzo alitoa changamoto kwa viongozi kuwafikiria Wakenya kwanza kabla ya kufanya maamuzi yoyote akiongeza kuwa siasa za hadaa na migawanyiko hazina nafasi.

Aidha amelitaka kanisa kukumbuka nchi katika maombi dhidi ya ukatili ikiwemo kuongezeka kwa visa vya kutekwa nyara kwa wakenya wasio na hatia.

Alibainisha kuwa Wakenya wasio na hatia wamekuwa wakitekwa nyara na kuteswa kabla ya kuachiliwa.

“Tunalaani visa vinavyoongezeka vya utekaji nyara na mauaji . Padri ombea viongozi was Kenya Kwanza ambao wako na roho mbaya sana, roho ya utekaji nyara, yaani mtu anateka mwenzake nyara anamweka ndani kwa Subaru anatoweshwa na kuteswa. Wanaoteka nyara ni wakenya, wanabeba bunduki ambazo zimenunuliwa na watu wa Kenya, tuombe huyo shetani aondoke Kenya hii,” alisema zaidi.

Maoni yake yaliungwa mkono na kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa aliyesema kuwa kama viongozi wa upinzani wanasimama na Kanisa Katoliki kudai uwajibikaji kutoka kwa serikali ya Kenya Kwanza na vita dhidi ya ufisadi.

Alisema kuwa kanisa linapaswa kuheshimiwa kwa kusema ukweli na kuongeza kuwa wale wanaolilaani kanisa hilo kwa kupiga vita rushwa wanapaswa kuacha na kujitathmini upya.

Bw Wamalwa alibainisha kuwa katika uchaguzi mkuu ujao, Wakenya wanapaswa kuwapigia kura viongozi ambao wana tabia nzuri wala si waongo na walio na sifa za kutiliwa shaka.

“Tunasimama na kanisa kwa vile wanataka nchi irudi kwenye utawala wa sheria sio utawala wa uongo, kama umekuwa ukiwadanganya Wakenya uchaguzi ujao Wakenya watasimama na kusema hapana kwa uongo na viongozi ambao wamekuwa wakihusika na ufisadi. Tuna kiongozi kama Kalonzo Musyoka, angalia rekodi yake, na ukichunguza kwa makini hana rekodi mbaya,” alisema Wamalwa.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA

 

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*