Uhuru aunga Gen Z katika kampeni ya kutetea haki – Taifa Leo


RAIS Mstaafu Uhuru Kenyatta kwa mara ya kwanza amevunja kimya chake kuhusu maandamano ya Gen Z, akiwataka waendelee kutetea haki zao.

Akizungumza kwenye hafla ya mazishi ya binamu yake, Kibathi Muigai aliyezikwa jana nyumbani kwake Gatundu Kusini, Kaunti ya Kiambu, Bw Kenyatta alitoa matamshi yanayofasiriwa kama kuunga mkono maandamano ya vijana nchini kwa kuwahimiza kujitokeza kupigania haki zao.

Rais huyo wa nne wa Jamhuri ya Kenya, alisema vijana kwa sasa ndio wana nguvu na kwamba, hawana budi kupambana na wanaowahujumu.Bw Kenyatta alihimiza vijana kuendelea na ukakamavu na ujasiri walioonyesha mwaka uliopita, 2024, kufuatia maandamano ya kitaifa waliyoshiriki.

“Mpiganie haki yenu bwana, sio kukaa hapo mali yenu ichukuliwe… Mmeitolea jasho, msikubali… Pambaneni mhakikishe mmepata haki yenu. Mnaskia nyinyi?” Bw Kenyatta alisema.

Akiomboleza Bw Kibathi, Rais huyo mstaafu alimtaja kama kiongozi jasiri ambaye hakuogopa kutetea haki za watu wake na taifa kwa jumla.Mnamo 1988, kumbukumbu zinaonyesha aliyekuwa Rais wakati huo, Daniel Arap Moi – ambaye kwa sasa ni marehemu, alimrusha jela kwa kipindi cha miaka sita Bw Kibathi kwa tuhuma za kushirikiana na upinzani katika njama ya kumng’oa mamlakani.

Kibathi, mwaka huo alikuwa na umri wa miaka 35 na alikuwa mtoto wa kiume wa Mzee James Muigai, nduguye Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Kenya, Mzee Jomo Kenyatta. Kibathi alirushwa katika jela la Kamiti, Nairobi.

Kando na kuwa mtetezi wa raia, Kibathi pia alikuwa mwendesha magari ya Safari Rally.Bw Kenyatta aliwataka Gen Z kuwa na ujasiri kama wa binamu yake katika kuhakikisha wanatetea mali yao dhidi ya kupunjwa.

“Hamuwezi mkakaa hapo tu na kuruhusu watu watumie vibaya mali mliyotolea jasho kutafuta. Dunia haiendi namna hiyo. Muwe watu ambao hamtaogopa, muishi kama rafiki yangu ( Kibathi Muigai). Alipelekwa kizuizini, si alitoka na akaendelea na maisha?” alihoji.

Katika maandamano ya mwaka jana ambayo yalitikisa nchi, Gen Z walijitokeza katika kila kona ya nchi kupinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024 ambao baadaye Rais William Ruto aliufutilia mbali kutokana na presha na ghadhabu za vijana. Rais pia alilazimika kuvunja baraza lake la mawaziri na kuteua jipya wakiwemo, washirika wa kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Akionekana kumiminia sifa vijana wa Gen Z, Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta aliwahimiza wasitishwe na yeyote kutetea haki zao. “Shida ya watu siku hizi…kila mtu…sijui mumeogopeshwa. Hata wewe Ngina…rudi uingie hii…MaGen Z nyinyi ndiyo stori ya siku za usoni,” Bw Kenyatta alisema. Ngina, ni bintiye Kenyatta.

Vijana wakiandamana Jijini Nairobi, Alhamisi, Juni 20, 2024. PICHA|BONIFACE BOGITA

Rais huyo mstaafu aliendelea kutia vijana motisha, akiwataka wafahamu kwamba hakuna shida zinazodumu.“Kila kitu kinataka kupiganiwa. Kikienda, mtu asilie. Msimame mpiganie haki yenu, na kwa wazazi mko na hawa watoto wamebaki ambao wako tayari kupigania haki yao waungane pamoja nanyi,” alisema.

Kwenye matamshi yake yanayoashiria anaunga vijana kushiriki maandamano, Bw Kenyatta alisema: “Hata nyinyi teteeni haki zenu…sio kukaakaa tu mnaogopa…kuogopa sasa ni sisi, sisi tutulie. Nyinyi ndio mko na nguvu ya kupambana na hii watu. Tuko nyuma yenu, na muendelee namna hiyo.” Wakati wa maandamano ya Gen Z, baadhi ya wandani wa Rais Ruto walimlaumu Bw Kenyatta kwa kufadhli machafuko.

Matamshi ya Bw Kenyata yanayochukuliwa anaunga mkono msimamo wa Gen Z yanajiri mwezi mmoja baada ya Rais Ruto kumtembelea Rais huyo mstaafu na kumtuza mbuzi 12 kama ishara ya kujaribu kuomba msamaha madhila aliyofanyiwa.

Kauli yake inajiri siku ambayo baadhi ya wandani wake Mutahi Kagwe na Lee Kinyanjui waliapishwa baada ya kujiunga na baraza la mawaziri la Ruto.

Rais William Ruto amekuwa akikosoa vijana akisema wamepotoka hasa kwa kutumia mitandao ya kijamii kuendeleza uasi dhidi ya serikali yake.Baadhi ya vijana wamekuwa wakitekwa nyara na kuzuiliwa kwa muda bila kujulikana waliko kwa kuchapisha jumbe na michoro inayolenga serikali na maafisa wake.

Utekaji nyara wa hivi karibuni umewalenga zaidi vijana waliomkosoa Ruto kwenye mitandao ya kijamii, huku makundi ya kutetea haki za binadamu yakionekana kutokubaliana na polisi ambao wamekanusha kwamba hawahusiki katika utekaji nyara huo na kuomba hatua zichukuliwe.

Akizungumza mbele ya umati wa watu huko Homa Bay, Ruto aliahidi kukomesha vitendo vya utekaji nyara lakini aliwaambia pia wazazi kuwajibika katika malezi ya watoto wao.

“Tutakomesha utekaji nyara ili vijana waishi kwa amani,” alisema na kuongeza wazazi wanapaswa kuwaonya watoto wao wawe na maadili. Baadaye vijana watano kati ya saba waliotekwa Desemba waliachiliwa huru.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*