Uhusiano tata wa Chebukati na Ruto, Uhuru na Raila – Taifa Leo


IWAPO aliyekuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati – aliyeaga dunia Alhamisi, Februari 20, akiwa na umri wa miaka 63 – angerejea maisha yake, kuna uwezekano kwamba hangechagua kuongoza tena tume hiyo.

Uchaguzi nchini Kenya, ni uwanja wa vita kwa wanasiasa wanaoungwa mkono na wafuasi wanaokataa kushindwa, na kusimamia tume ni kazi ya kutisha.

Katika kitabu chake, Referee of a Dirty Game (Refa wa Mchezo Mchafu), aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Issack Hassan, ambaye alifukuzwa ofisini mwaka wa 2016, anasema ni kazi isiyo na shukrani, haswa unapokabiliana na wanasiasa wenye majina makubwa. Mrithi wake Chebukati alijifunza hili kwa njia ngumu.

Kwa Bw Chebukati, muhula wake wa miaka sita katika IEBC ulimfanya kuhusiana na watu mashuhuri kisiasa, hasa Dkt William Ruto, Bw Uhuru Kenyatta, Bw Raila Odinga -viongozi ambao maoni ya wafuasi wao dhidi ya mkuu wa tume ya uchaguzi mara nyingi yalifanana na ya wanasiasa. Mambo yalikuwa magumu hasa baada ya uchaguzi wa urais uliozozaniwa wa 2007 uliosababisha ghasia mbaya zaidi za kisiasa nchini Kenya na kusababisha mageuzi.

Hata hivyo, Bw Chebukati alitangaza mara kwa mara kuwa alikubali changamoto hiyo na kusimamia Uchaguzi Mkuu wa 2017 na 2022 ambao ulikuwa na utata.

Uchaguzi wa urais wa 2017, ambao Uhuru Kenyatta alimshinda kiongozi wa upinzani Bw Odinga ambaye alipinga matokeo hayo, ulibatilishwa na Mahakama ya Juu. Jaji Mkuu wa wakati huo David Maraga alisema haukutimiza kipimo cha sheria. “Ukiukaji wa sheria” ulioelezwa na mahakama ulisababisha marudio ya uchaguzi mnamo Oktoba mwaka huo, ambao Kenyatta alishinda kwa urahisi na baada ya Bw Odinga kuususia.

Mwenyekiti wa IEBC Chebukati alipinga wito wa kujiuzulu na akaongoza uchaguzi wa 2022 ambapo Bw Kenyatta wakati huu alimuunga mkono Odinga dhidi ya naibu wa rais wakati huo Ruto. Ni uchaguzi uliogawanya tume hiyo katikati huku Dkt Ruto akiibuka mshindi asiyetarajiwa.

Kura ya 2022 haikuwa tu kinyang’anyiro kingine cha uchaguzi – vilikuwa vita vya chuki za kisiasa za muda mrefu ambazo ziliweka Bw Chebukati na timu yake katika ya shinikizo kubwa.

Kabla ya uchaguzi wa 2017, kambi ya Bw Odinga haikuwa na maneno mazuri kwake huku mrengo wa UhuRuto mara nyingi ukitetea IEBC, tume ambayo ilikumbwa na mgawanyiko ambao ulikuwa mbaya zaidi,

Kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022, Bw Chebukati alikuwa mtu mashuhuri, Dkt Ruto na Bw Odinga wakimchagua yeye na IEBC kulaumiana.

Uhusiano wa Bw Odinga na Bw Chebukati, ulianza mapema zaidi. Mnamo 2007 Chebukati aligombea kiti cha ubunge cha Saboti kwa tikiti ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kwa na kupoteza kwa Eugene Wamalwa wa PNU.

Baada ya kupoteza, Bw Chebukati alijiuzulu kutoka ODM ya Bw Odinga. Mnamo 2017, Bw Odinga alitumia kubatilishwa kwa uchaguzi kama thibitisho IEBC ilipendelea Rais Kenyatta na Bw Ruto.

Bw Odinga alitoa wito wa mageuzi na akajiondoa katika marudio ya uchaguzi wa urais wa Oktoba 2017 wakati matakwa yake hayakutekelezwa.

Kwa muda, haswa mnamo 2018 baada ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kuwa na handisheki Naibu Rais Ruto alimshuku Bw Chebukati na timu yake ya IEBC.

Wakati mmoja mnamo Agosti 2018 alidai Bw Chebukati alikuwa akifanya mikutano ya usiku na kambi ya Bw Odinga, wakati huo ikijulikana kama National Super Alliance (Nasa).

‘Nina habari kwamba Chebukati anakutana na viongozi wa NASA usiku. Hiyo inaweza kuwa ndiyo sababu anatuma jumbe za hapa na pale. Ninamuomba akomeshe hayo na azingatie kuwasilisha uchaguzi wa kuaminika,’ Dkt Ruto alisema.

Ni shtaka ambalo Bw Chebukati alikanusha kuwa la ‘uongo, la zembe na lisilo na msingi’ lakini madai ya mikutano hiyo ya kisiri na kambi tofauti yaliendelea wakati wa maandalizi ya uchaguzi wa 2022.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*