CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kinakabiliana na mgawanyiko mpya wa ndani kutokana na makubaliano ya kisiasa kati ya kinara wake Raila Odinga na Rais William Ruto ambayo yalishuhudia viongozi wakuu wa chama hicho kuteuliwa serikalini.
Mgawanyiko huo unatokana na kauli zinazokinzana za washirika wa Bw Odinga kuhusu hatua ya kuunga mkono utawala wa Kenya Kwanza na uwezekano wake kuchaguliwa tena.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ODM, Junet Mohamed, aliandamana na Dkt Ruto kwa ziara ya pwani wiki hii ambapo aliwakashifu wakosoaji wa serikali.
Bw Mohamed alionekana kujiunga na wenzake wa zamani katika ODM ambao walijumuishwa katika baraza la mawaziri mnamo Julai, ambao wametangaza kuwa wataunga mkono serikali ya Dkt Ruto.
Wao ni pamoja na; waliokuwa naibu viongozi wa chama cha ODM Hassan Joho na Wycliffe Oparanya, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM John Mbadi na aliyekuwa Katibu wa Masuala ya Kisiasa Opiyo Wandayi pamoja na aliyekuwa mwanachama wa bodi ya uchaguzi ya chama hicho Bi Beatrice Askul.
Ingawa yeye si miongoni mwa mawaziri hao watano, hatua ya Bw Mohamed kutetea serikali inaonekana kuwakera baadhi ya wanachama wa ODM.
“Tusiwe nchi ya kulalamika peke yake kwa sababu nina haki ya kusema chochote ninachotaka. Huwezi kufunga mdomo wangu. Mdomo ni wangu na siasa ni yangu. Tumekubaliana kwamba ikiwa serikali inafanya kile kilicho katika manifesto yetu, hakuna cha kupinga,” Bw Mohamed alisisitiza.
Lakini Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna Jumatano alisisitiza kuwa chama hicho kinasalia katika upinzani, akiongeza kuwa yeye ndiye msemaji rasmi wa chama hicho.
“Hatuna mkataba wowote na UDA na hatuko serikalini. Ninataka kusema kuwa Katibu Mkuu ndiye msemaji rasmi wa chama na huzungumza baada ya mijadala na vyombo vya chama,” akasema Bw Sifuna.
Alisema kuwa hatua ya waliokuwa maafisa wa ODM kujiunga na baraza la mawaziri haimaanishi kuwa chama hicho pia kimejiunga na utawala wa Kenya Kwanza.
“Sababu iliyonifanya kutohudhuria hotuba ya Rais kuhusu Hali ya Taifa ni kwa sababu Ruto hawezi kuaminiwa na siamini kwamba anazungumza ukweli,” Bw Sifuna alisema alipokuwa akihojiwa na Radio Citizen Jumatano asubuhi.
Huku wakiandamana na Rais Ruto Pwani, Bw Mohamed, Bw Joho na Opiyo Wandayiwalitetea serikali, na kuapa kuunga mkono kuchaguliwa tena kwa rais 2027.
Bw Mohamed hata hivyo, alishikilia kuwa kulingana na katiba, yeye ndiye kiongozi mwaminifu wa upinzani kwa sababu ya nafasi yake ya Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa.
Naibu Kiongozi wa ODM Godfrey Osotsi mnamo Jumanne alisema bado wana miaka miwili na nusu hadi 2027 na mazungumzo ya kuunda muungano yatakuja na watashughulikia kila kitu hatua kwa hatua.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply