Una haki kisheria kushtaki mwanandoa mwenzako akikusababishia jeraha – Taifa Leo


UNAWEZA kumshtaki mumeo au mkeo akikupiga na kukusababishia jeraha. Waathiriwa wengi wa dhuluma za nyumbani huwa wanakosa kuchukulia wanaowadhulumu hatua pengine kwa kutofahamu ni haki yao ya kisheria kufanya hivyo au kwa kukosa msaada.

Mtu anaweza, au anafaa kuchukulia yeyote anayemdhulumu kimwili hatua za kisheria kwa kuwa ni uhalifu kushambulia mwingine.

Hatua ya kwanza ni kuripoti kisa kwa polisi au maafisa wa utawala baada ya kudhulumiwa na kupata matibabu. Bila shaka hatua ya kwanza ni kupata matibabu na kisha kuelekea kituo cha polisi.

Polisi huwa wanapatia mwathiriwa Fomu inayofahamika kama P3 ambayo huwa inajazwa na daktari wa polisi kuelezea kiwango cha majeraha. Fomu hii ni muhimu na inafaa kulindwa isiharibike au kupotea kwa kuwa inatumiwa kama ushahidi kortini.

Kwa kutumia nguvu za Fomu hii, mwathiriwa anaweza kusababisha anayemdhulumu kukamatwa na kufikishwa kortini kufunguliwa mashtaka.

Hata hivyo, ni muhimu kupima uhusiano wako na mchumba anayekushambulia kwa kuwa kesi ikifika kortini inaweza kuwatenganisha.Dhuluma za kinyumbani  zinaendelea kuongezeka kwa kuwa watu wengi hawachukulii hatua za kisheria wanaowatendea ukatili.

Ripoti za mashirika tofauti zinaonyesha kuwa idadi ya watu wanaodhulumiwa na wachumba wao inazidi kuongezeka kila siku. Mwaka wa 2023, takwimu za idara ya polisi pia zilionyesha kwamba kesi za dhuluma za kinyumbani zinaripotiwa kila siku katika vituo vya polisi kote nchini.Mashirika ya kijamii yanasema idadi kubwa ya wanaodhulumiwa ni wanawake.

Ripoti moja ya chama cha mawakili wanawake nchini (FIDA) inasema  kwamba visa vya dhuluma za kinyumbani ni kubwa kuliko inavyodhaniwa.
Shirika hilo linasema hii ni kwa sababu watu wengi huogopa kuripoti wanapodhulumiwa na wachumba wao.

“Watu wengi huamua kuteseka kimyakimya tu. Wanaogopa kuripoti  wanapodhulumiwa ili waepuke fedheha kutoka kwa jamii,” yasema sehemu ya ripoti hiyo.

Ripoti nyingine ya shirika la Coalition for violence against women inalaumu mila na desturi za kiafrika kwa ongezeko la dhuluma hizi.

Inasema jamii nyingi za kiafrika zinaamini kwamba mwanamke ni chombo kinachofaa kutumiwa na mwanaume.Sheria ya ndoa ya Kenya inatoa adhabu kwa wanaodhulumu wake, waume au watoto wao.

Hakuna makosa kutoroka mwanandoa anayekudhulumu na kuomba talaka. Dhuluma ni ukatili na ni moja ya sababu zinazoruhusiwa kuwasilisha kesi ya talaka.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*