Unakosa hekima kwa kunyima mkeo ruhusa ya kufanya kazi – Taifa Leo


WAPO wanaume wanaowakandamiza wake wao, kuwafinyilia na kuwanyima uhuru wa aina yoyote kama wa kutafuta mali.

Lakini ikiwa mwanamume anataka kufaulu maishani, ni vyema kumruhusu mke wake kutafuta mali ana asikandamize haki yake ya kupata mali. Amhimize na kumsaidie kupata mali akiona ana ari ya kuitafuta.

Kumnyima mke fursa ya kupata mali ni kujinyima ufanisi. Anayefanya hivi ni mwanamume anayeishi karne kadhaa zilizopita. Wanaume wa siku hizi wanataka wanawake wenye bidii sio wanaolaza damu.

Kunyima mkeo nafasi ya kutafuta mali yake binafsi kunaonyesha unamshuku, haumuwazii mema na kwamba haumwamini.

“Kuna wanaume wanaoamini kuwa wake wao hawafai kumiliki mali yao binafsi, imani ambayo imepitwa na wakati. Hakuna kinachozuia mwanamke anayejitafutia mapato kwa bidii na jasho lake kununua gari, mashamba, nyumba au kujenga ploti na kujiwekea akiba,” asema mshauri wa masuala ya ndoa, Brian Githome. Anahimiza wanandoa kushirikiana kutafuta mali

“Japo hakuna sheria inayoamrisha iwe hivi, kwa sababu ya tandabelua la kuvunjika kwa ndoa siku hizi, utakuta mume na mke kila mmoja anaamua kumiliki mali yake binafsi. Hii inakinga mtu iwapo janga la talaka litamwangukia apigwe teke na kujipata mikono mitupu,” asema na kuongeza kuwa ni haki ya kila mtu kutafuta mali yake binafsi awe katika ndoa au la.

Wanandoa wanaotambua na kuheshimu haki za kimsingi za kila mmoja kutafuta mali, huwa wanaishi kwa amani bila bughudha na mivutano inayotokea.

“Mivutano kama mume kukataa kutunza watoto wake akiwa na uwezo wa kufanya hivyo na kutumia mali yake kulewa au kwa mipango ya kando ni ujinga usiofaa kusamehewa unaofanya wanawake kuamua kujitafutia mali,” asema.

Mwanamume mwenye hekima huwa anaruhusu mkewe kutia bidii kutafuta mali kwa kuwa kitu chochote kikifanyika huwa wa kwanza kunufaika nayo.

“Hofu ya wanaume wanaozima wake wao kutafuta mali ni kuwa wakiomoka watawapiga teke. Haya ni mawazo ya wanaume wazembe na waliopungukiwa na hekima kwa kuwa hofu hii imelindwa katika sheria ya ndoa ya Kenya inayopatia wanandoa haki ya kugawana mali waliyopata katika muda ambao wamekuwa mtu na mke au kurithi mali ya wachumba wao wakiaga dunia,” asema Githome.

Anasema sheria inampatia mtu haki ya kumiliki mali ambayo mkewe au mumewe alipata katika kipindi cha ndoa yao.

“Hofu hii haina mashiko kwa sababu katika ndoa, mume na mke huwa wanapatiana haki zao za mapenzi ikiwemo tendo la ndoa. Ikiwa basi unadai haki ya tendo la ndoa kutoka kwa mume au mke wako na anakupatia bila masharti hadi unaridhika, kwa nini unamnyima haki ya kumiliki mali ambayo asipokuwepo itakuwa yako,” anahoji mtaalamu huyu.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*