NI Krismasi, jibambe, lakini uwe mwangalifu. Hii ni kwa wale wanaotumia siku hii kwa starehe.
Wakijumuika katika kumbi za starehe kwa burundani licha gumzo za kawaida siku zilizotangulia kwamba hali ya uchumi imekuwa mbaya mwaka huu.
Pengine kabla ya kuingia kwa klabu kutumia mamia au maelfu kadhaa kwa vileo wanafaa kutafakari kuhusu hali waliyopitia mwaka huu na mipango ya mwaka ujao hasa walio na watoto wa kulipia karo au watu wanaowategemea.
Ni wazi kuwa hali ngumu ya uchumi haiishi na krismasi au mwaka huu. Itakuwepo mwaka mpya na itakuwa ngumu zaidi kwa wale watakaojibamba kiholela.
Sio tu kwa kuwa wako na watu wa kuwategemea itawalemea zaidi wakidhurika kiafya kwa kuzidisha starehe.
Gharama ya huduma za afya ni ile ile. Watakapogutuka watapata mfumo wa Bima ya Afya ya Jamii haujaanza kufanya kazi ilhali watakuwa wamemalizia pesa kwa starehe za Krismasi zinazobadilika kuwa balaa.
Starehe za siku chache hazifai kuharibu mipango ya siku zijazo. Hizi ahadi kwamba maisha yatakuwa nafuu mwaka ujao ni hekaya kwa sasa. Ni jambo la kufuatilia kwa subira.
Kuombea nchi ni muhimu msimu huu. Tusidanganyane, mazingira sio mazuri na wataalamu huru wa sekta mbali mbali wametufahamisha hivyo.
Hata hivyo, wale wanaoamini katika nguvu za maombi ya dhati kama mimi. Wale wanaoamini kwamba Mungu ana njia zake za kuauni watu wake hata hali ikiwa tete zaidi, huu ni wakati wa maombi.
Furahia Krismasi kwa kuwa ni haki kufanya hivyo lakini kwa kiasi. Pengine la busara ni kusambazia wasichonacho kidogo ulichonacho, wapate tonge la kutia tumboni, huenda ikawa ufunguo wa baraka mwaka ujao.
Leave a Reply