ALIYEKUWA kiongozi wa kundi haramu la Mungiki Maina Njenga anaonekana kuendelea kuandamwa na maovu ya kundi hilo anapoanza kuwania viti katika ulingo wa siasa.
Licha ya Bw Njenga kutangaza kuwa amekatiza uhusiano wake na kundi la Mungiki na kujaribu kuwania nyadhifa za kisiasa, kwa miaka 20, hajaweza kufaulu.
Aidha, ametangaza kuwa anawania wadhifa wa kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao, 2027, na huenda uvundo wa Mungiki ukaathiri ndoto yake mara nyingine.
Hii ni kwa sababu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, mwenye ushawishi mkubwa katika eneo la Mlima Kenya, amedai kuwa analenga kufufua kundi hilo lililosababisha maafa na mahangaiko kwa wakazi wa eneo hilo.
Aidha, Bw Njenga ameendelea kuhusishwa na Mungiki katika mahojiano kati yake na wanahabari na shughuli zake za kisiasa.
Kwenye mahojiano yake na Taifa Leo nyumbani kwake eneo la Kitengela, Bw Njenga pia alizungumzia madai yaliyoibuliwa na baadhi ya viongozi kwamba anatumiwa na Rais William Ruto anayekabiliwa na upinzani mkubwa katika eneo la Mlima Kenya.
Bw Njenga hata hivyo, aliihakikishia Taifa Leo kwamba hajakodiwa na Rais Ruto amsaidie kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, akisisitiza kuwa lengo lake ni kuhakikisha kuwa watu wa eneo la Mlima Kenya wanapata nafasi katika afisi kuu serikalini.
Alikana madai ya kupokea fedha kutoka kwa serikali kuendeleza mpango wa kumhujumu Bw Gachagua katika ngome yake ya Mlima Kenya.
Anayedai kuwa ninalindwa na serikali hajui kile anachosema. Sihitaji usaidizi kutoka kwa mtu yeyote kufanya kile ambacho ninalenga kufanya mradi sijihusishi katika uhalifu
“Mimi si mradi wa Rais Ruto katika Mlima Kenya,” akasisitiza akifichua kuwa hajawahi kukutana ana kwa ana na Rais tangu Kenya Kwanza ilipoingia mamlakani.
“Unajua wazi kwamba katika uchaguzi mkuu uliopita, nilimuunga mkono Raila Odinga, aliyepoteza. Tulikubali kushindwa na tukaamua kuendelea na maisha,” Bw Njenga akaeleza.
Alisema kuwa ziara zake za hivi majuzi katika eneo la Mlima Kenya hazikuungwa mkono na wanasiasa ila ameamua kutumia ushawishi wake kuhakikisha kuwa wakazi wanafaidi kutoka kwa serikali.
Bw Njenga anashikilia kuwa yeye ni mtu tajiri na anaweza kufadhili shughuli zake za kisiasa, bila kusaka usaidizi kutoka kwa mtu yeyote.
“Baada ya Gachagua kutimuliwa kutoka serikali, haimaanishi kuwa watu kutoka Mlima Kenya wamekatiza uhusiano na serikali. Gachagua ni mtu mmoja tu miongoni mwa wakazi wengi wa Mlima Kenya. Hapo ndio nyumbani kwake, hapo ndio biashara zetu ziko. Mbona mtu fulani aniambie kuwa sifai kutembelea eneo ambako nilizaliwa?” akauliza.
“Nimeamua kuhakikisha kuwa watu wetu kutoka eneo hili hawapotezi na kwamba masilahi yao yanaendelea kushughulikiwa na serikali,” akaongeza. Hata hivyo, Bw Njenga anaweka wazi kuwa hamna uhasama wowote wa kibinafsi kati yake na Bw Gachagua.
IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA
Leave a Reply