Vijana wakatae mbegu ya ukabila inayopandwa na wanasiasa wenye ubinafsi – Taifa Leo


WAKATI vijana wa Kenya waliungana kukataa Sheria ya Fedha 2024, hawakujitambua kwa makabila yao.

Walisema waliunganishwa na lengo moja -kuepushia Kenya sheria kandamizi ambayo ilinyima wazazi wao mapato ya kutunza familia.

Kwao, ushuru ulioanzishwa kupitia mswada huo ulikuwa sumu na wabunge walioungana kuupitisha wakawa maadui wao.

Vijana hao, kwa ari na azma kuu, uzalendo na ujasiri, walijitenga na viongozi wa kisiasa na hata kidini kufanya walichoamini kilikuwa bora kwa nchi bila uongozi, kuegemea mrengo wowote wa kisiasa au kabila na umoja wao ulizima sheria iliyokusudiwa.

Hawakuhitaji kuvamia majengo ya bunge na hili linaalaniwa na yeyote mwenye busara. Hawakufaa kuuawa wakiandamana kwa amani barabarani zaidi ya 60 walivyofanyiwa.

Ilikuwa haki yao, kuandamana kwa amani kulalamikia serikali na tabia ya wanasiasa ya kupuuza wapigakura na kuwekwa makwapani na watawala.Na kwa sasa, viongozi wa kisiasa, kwa nia ya kuharibu maazimio ya vijana na nguvu zao wameanza kupanda mbegu ya ukabila miongoni mwa kizazi kilichokuwa na matumaini makuu.

Kizazi cha vijana ambacho kwa miezi michache kilidhihirisha ukabila unaweza kuangamizwa kinalengwa ili kigawanywe kwa misingi ya jamii zao.

Haya yanaonekana wazi kupitia matamshi ya viongozi wanayorushia wanaowachukulia kuwa wapinzani wao wasiotoka jamii zao.Yanadhihirika kupitia vitendo vya kutenga watu kutoka baadhi ya jamii katika uteuzi na uajiri serikalini.

Vijana wakikosa kuangukia mtego huu na kuungana kwa lengo moja, wakikataa kuvutwa katika injili ya ukabila na kimaeneo, watakuwa fahari ya nchi yao.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*