VIJANA kutoka eneo la Kati nchini wameitaka serikali kuunda wizara huru itakayoshughulikia masuala yanayowahusu.
Wakizungumza wakati wa kikao cha kushirikisha umma kuhusu Mswada wa Vijana wa 2024 mjini Nyeri, vijana hao kutoka Kaunti za Embu, Kirinyaga, Nyandarua, Nyeri na Murang’a, walisema wizara hiyo itahakikisha masuala yao yanatatuliwa kwa haraka, tofauti na hali ya sasa ambapo masuala ya vijana yameunganishwa na sekta nyingine.
Bi Florence Kiburu kutoka Kirinyaga, alisema kuwa kwa sasa kuna dosari katika mawasiliano, jambo ambalo limeathiri ushiriki wao katika masuala ya kitaifa.
“Serikali inazungumza lugha ambayo vijana hawaielewi. Vijana ni bomu linalosubiri kulipuka, na ningependa kushauri serikali kubuni mbinu bora za kuwasilisha taarifa zinazowahusu vijana. Pia, inapaswa kubuni mkakati wa kuwaunganisha vijana katika shughuli za kijamii na kutuwezesha kushiriki katika ujenzi wa taifa,” alisema Bi Kiburu.
Kulingana na Katibu Msimamizi katika Idara ya Masuala ya Vijana na Uchumi Bunifu, Allan Macharia, mara tu mswada huo utakapokuwa sheria, utachochea maendeleo ya vijana, ushiriki wao na kuwawezesha.
Mkurugenzi wa maendeleo ya vijana anayeshughulikia sera na utafiti katika idara ya vijana na uchumi bunifu, Dkt Josphine Etenyi, alisema hakuna sheria ya bunge inayoongoza ajenda ya vijana nchini.
Mswada huo, alisema, umeanzisha Hazina ya Vijana kurithi Hazina ya Maendeleo ya Biashara ya Vijana ambayo imekuwepo.
Dkt Etenyi alisema hii itasaidia kuimarisha hazina ya vijana ili kukidhi mahitaji ya mipango mingi ya vijana ikiwa ni pamoja na ujasiriamali, na kujenga uwezo wa ujuzi unaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri kwa maisha endelevu.
Mswada wa vijana pia unapendekeza kuundwa kwa ofisi ya Msajili ambayo itapewa mamlaka ya kusajili mashirika ya vijana na itapewa mamlaka ya kusuluhisha masuala yanayoathiri mashirika.
Akizungumza katika hafla ya kushirikisha umma katika Kaunti ya Kisii, Dkt Etenyi alisema mswada huo pia utakuwa na mpango wa tuzo kwa vijana katika tasnia ya ubunifu ambao utawatambua wale wanaofanya vyema katika vipaji ili kuwawezesha zaidi.
Aliwataka vijana kushiriki ipasavyo ili kuufanya mswada huo kuwa bora zaidi.
Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA
Leave a Reply