VIONGOZI wa Serikali, Mahakama na Watetezi wa Haki za Kibinadamu, jana walimuomboleza Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR), Roseline Odhiambo Odede aliyefariki dunia Ijumaa.
Rais William Ruto alimtaja Bi Odede kama mpiganiaji shupavu wa haki za binadamu nchini.
“Nimehuzunishwa mno na kifo cha Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya Roseline Odhiambo Odede. Alikuwa bingwa wa kustaajabisha wa haki za binadamu na mwanaharakati mashuhuri wa jamii iliyo sawa na haki,” Rais Ruto alichapisha kwenye akaunti yake ya X.
Jaji Mkuu Martha Koome ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Usimamizi wa Haki ambapo Odede aliwahi kuwa mwanachama alisema marehemu alikuwa mtu ‘wa kipekee’.
“Michango yake ya kipekee katika kukuza na kulinda haki za binadamu na kuimarisha usimamizi wa haki nchini itatutia moyo milele, na urithi wake utaendelea kuangazia njia kwa vizazi vijavyo,” Bi Koome alisema katika taarifa. Amnesty International Kenya ilimsifu kwa kupigania haki za binadamu nchini. “Katika miaka michache iliyopita, tumefurahia msimamo wake wa ujasiri dhidi ya ukiukaji wa haki za binadamu huko Yala, Nyalenda, Nyando, Shakahola, na wakati wa maandamano ya kitaifa 2024,” Mwenyekiti wa Amnesty International Kenya Dkt Stellah Bosire alisema.
Akitangaza kifo cha Bi Odede, Makamu Mwenyekiti wa KNCHR Raymond Nyeris alisema alifariki Ijumaa baada ya kuugua kwa muda mfupi.
“Kifo chake cha ghafla ni pigo kubwa kwa Tume na taifa kwa ujumla. Kama Tume tulipata fursa ya kuhudumu na Roseline Odede kama Mwenyekiti katika uongozi wa KNCHR,” Dkt Nyeris alisema. Bi Odede aliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuongoza KNCHR mnamo 2021.
Leave a Reply