MTANGAZAJI mkongwe Leonard Mambo Mbotela amekufa akiwa na umri wa miaka 84.
Mbotela, ambaye alijizolea umaafu kwenye anga ya utangazaji redioni, haswa kupitia kipindi chake cha “Je, Huu ni Ungwana?” alifariki jana asubuhi.
Mmoja wa wanawe wa kiume, Jimmy, aliambia Taifa Leo kwamba mtangazaji huyo aliaga dunia katika Hospitali ya Nairobi alikolazwa baada ya kuugua.
Kupitia sauti yake ya kuvutia na umilisi wake wa lugha ya Kiswahili, Mbw Mbotela alifahamisha Wakenya kupitia habari za mada mbalimbali ikiwemo spoti.
Aliwashambulia watu wenye mienendo mibaya kupitia kupindi chake maarufu cha “Je, Huu ni Ungwana?” alichokipeperusha kupitia idhaa ya Kiswahili ya redio ya Shirika la Utangazaji Nchini (KBC) na baadaye runinga ya KBC TV.
Aidha, alikuwa mtangazaji mashuhuri wa kandanda na sauti yake iliwapendeza wengi.
Jana, Rais William Ruto alimkumbuka Mbotela kama mtangazaji “aliyejaliwa kipawa cha sauti iliyovutia akitangaza mpira na kupeperusha kipindi chake maarufu cha “Je, Huu ni Ungwana?”.
Bw Mbotela alizaliwa katika hospitali ya Lady Grigg mjini Mombsa mnamo Mei 29, 1940 na alikuwa kifungua mimba katika familia yake.
“Nilipewa jina Leonard kutokana na jina la Mmishenari wa Uingereza, Askofu Leonard Beecher. Mmishenari huyu alimfundisha babangu katika Shule ya Upili ya Alliance mnamo 1926,” akaandiki katika tawasifu yake “Je, Huu ni Uungwana?: Kumbukumbu ya Leonard Mambo Mbotela”.
Kwenye dibaji ya kitabu hicho, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi anatoa muhtasari wa stori ya Mbotela kama “mvulana aliyezaliwa Freretown, Mombasa na akakua katika eneo la Ukambani, akafanya kazi Bonde la Ufa na kukita kambi Nairobi kuwafurahisha mamilioni ya wasikilizaji kutoka studio za KBC.
Bw Mbotela alijiunga na fani ya utangazaji mnamo 1963, Kenya ilipopata uhuru.
Alikuwa mtangazaji wa habari, kandanda, mwalimu wa Kiswahili kwenye redio na mtetezi wa maadili katika jamii kupitia kipindi chake cha “Je, Huu ni Uungwana?” alichokiazisha mnamo 1966.
Aidha, alipeperusha matangazo ya kibiashara kwenye redio kwa lugha ya Kiswahili na alihudumu kama mtangazi katia Shirika la Habari za Rais (PPS).
Kwenye tawasifu yake Mbotela aliandika kuwa ilikuwa fahari yake kuwa mwanahabari kwa sababu hiyo ndio ilikuwa ndoto yake kuu maishani.
“Nilitaka kuwa mtangazaji. Singetaka kufanya kazi nyingine kando na kuwa katika kituo cha redio. Hii ndio ilikuwa ndoto yangu,” akasema.
Mojawapo ya nyakati za kuu katika maisha ya Mbotela ilikuwa kwamba mnamo 1982 alilazimishwa na wanajeshi kutangaza kuwa Rais Daniel Moi alikuwa ametimuliwa mamlakani..
Wanajeshi hao waasi, ambao jaribio lao lilifeli, walitaka kutumia sifa na imani ya umma kwa Mbotela ili kufanikisha ajenda yao.
Naibu Rais Kithure Kindiki, Mkuu wa Mawaziri Bw Mudavadi, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, Kiongozi wa Azimio Raila Odinga na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ni miongoni mwa viongozi wakuu nchini waliotuma jumbe za kuomboleza Bw Mbotela.
Leave a Reply