HAKUNA haja ya kuwaamrisha vijana nchini wawe na maadili ilhali viongozi wenyewe ndio wakaidi wanaoonyesha kuwa hawana hekima kutokana na kauli zinazotoka kwenye vinywa vyao.
Kutokana na maasi ambayo yamekuwa yakiendelea mitandaoni dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza, baadhi ya wanasiasa wamekuwa wepesi wa ‘kuwapa msomo’ wazazi wawape vijana wao malezi bora.
Mitandaoni, vijana wamekuwa wakiweka michoro ya baadhi ya wanasiasa wakuu wakiwa kwenye majeneza pamoja na kuandika mambo mabaya kuwahusu.
Kiini cha hili ni changamoto za kiuchumi, uongo wa Rais William Ruto na visa vya utekaji nyara ambavyo vimekuwa vikiwalenga vijana hawa kutokana na machapisho yao mitandaoni.
Rais Ruto, Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga na baadhi ya viongozi wamejipata katika hali hii pamoja na mawaziri wengine ndani ya utawala huu. Utekaji huu umezidisha maasi hayo hasa baada ya serikali kudai kuwa haihusiki na visa hivyo na kuibua kitendawili zaidi kuhusu nani anashiriki uovu huo.
Hata hivyo, huwezi kuwadhibiti vijana na kuwakemea ilhali viongozi wakuu katika utawala huu ndio wana mazoea ya kutoa semi za chuki.
Viongozi wetu wanaonekana kutokuwa na mtazamo wowote kuhusu hali halisi nchini kutokana na kulewa mamlaka na kuwatapikia wananchi.
Majuzi mbunge wa Daadab Farah Maalim alivutia ghadhabu kutoka kwa vijana baada ya kuwatusi Wakenya, matusi yasiyochapishika kwa kudai kuwa Rais Ruto lazima aende nyumbani.
Kiongozi kama huyo anasimama kwenye mkutano wa rais ambaye naye anatabasamu tu huku Wakenya wakitusiwa. Yaani kwa mujibu wa Bw Maalim, 69 malipo ya Wakenya wanaotaka uongozi bora nchini ni kuwatusi matusi makubwa ?
Kama wazee kama Bw Maalim ambaye aliingia bungeni mnamo 1992 kwa mara ya kwanza kupitia Ford Kenya, amekuwa kwa siasa kipindi hiki chote na hata akawa naibu spika, basi tutarajie vipi vijana watawasikiza. Chama cha Ford Kenya alichotumia Bw Maalim alipokuwa akiingia siasa kilikuwa chama kilichofahamika kwa mageuzi na kupigania haki na inashangaza mwanasiasa huyu amechukua mwelekeo ambao hauambatani na alikoanzia siasa.
Mwaka jana wakati wa maandamano ya Gen Z ni huyu huyu Bw Maalim alisema kuwa angekuwa rais wa nchi, angeamrisha vijana 5,000 ambao walivamia Bunge la Kitaifa wauawe kikatili.
Je, vijana wanaweza kushauriwa na kiongozi kama huyu ambaye hutumia lugha chafu, haonekani kuheshimu umri wake mkubwa na huwatishia mara kwa mara? Kuna madai kuwa uaminifu wa Bw Maalim uko Somalia wala si Kenya na iwapo hilo ni kweli huenda ndiyo sababu ya kuwatupia vijana maneno ya kukera.
Kiongozi wa Wengi kwenye Bunge la Kitaifa, Kimani Ichung’wah pia ni mwengine ambaye amekuwa akipayukapayuka kwa kutoa matamshi ambayo hawezi kuthibitisha.
Bw Ichung’wah amekuwa akidai kuwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amekuwa akihusika na visa vya utekaji nyara ili kuiharibia sifa serikali.
Suala la watu kutekwa nyara si jambo ambalo linaweza kutumika kucheza siasa jinsi ambavyo Bw Ichung’wah amekuwa akifanya hata kama ana mamlaka makubwa katika utawala wa sasa.
Kinachosikitisha ni kuwa wanasiasa ambao wanastahili kuwa mstari wa mbele katika kuwakashifu vijana na kuwataka wawe na maadili ndio wale wale ambao wamekuwa wakisimama majukwaani na kuzungumza ‘matope’
Leave a Reply