ZIARA ya siku tano ya Rais William Ruto Magharibi mwa nchi ambayo ilikamilika mnamo Ijumaa, ilianika uhasama wa kisiasa eneo hilo huku viongozi wakijipanga kwa kura ya 2027.
Binafsi, Rais Ruto aliwakemea wapinzani wake katika kiny’ang’anyiro cha 2027 huku akiwalenga aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka.
Siasa za kieneo ziligubika ziara ya Rais Ruto kwenye kaunti za Kakamega, Bungoma, Vihiga na Busia huku baadhi ya viongozi wakizomewa na raia kutokana na utendakazi duni.
Katika Kaunti ya Kakamega, uhasama kati ya Mbunge wa Mumias Magharibi Johnson Naicca na mwenzake wa Mumias Mashariki Peter Salasya ulijitokeza wazi.
Mzee Naicca alimshutumu Bw Salasya kwa kudai kuwa Rais anapotoshwa na washauri wake.
“Ruto amekuja kuokoa kiwanda cha Mumias na shutuma kutoka kwa viongozi kama Salasya zitamvunja moyo. Hatutaki siasa mbaya zivuruge mpango wa kufufua kiwanda na Bw Salasya anastahili kujiunga nasi kumuunga Rais iwapo anataka kupiga hatua kisiasa,” akasema Mzee Naicca.
Pia vita vikali vya kisiasa vilizuka kati ya Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa, Senata Boni Khalwale na Mbunge Mwakilishi wa Kike Elsie Muhanda. Kulikuwa na kioja mjini Kakamega mbele ya Rais Ruto pale Bw Khalwale alimshutumu gavana kwa kulemewa na kazi akidai pia ni fisadi.
Bw Khalwale alidai Gavana Barasa amefyonza fedha ambazo aliyekuwa Gavana Wycliffe Oparanya (sasa wazi wa ushirika na biashara ndogo ndogo), alitengea ujenzi wa uga wa Bukhungu na Hospitali ya Level 6 ya Kakamega.
“Barasa, wewe ni ndugu yangu mdogo, rejesha taa za barabarani ambazo zilikuwa Kakamega na safisha mji ili kuondoa harufu mbaya. Pia inasikitisha kuwaona wanawake wanaofanya biashara rejareja kama kuuza uji wakifurushwa kwa kuondolewa kwenye biashara,” akasema Bw Khalwale.
Seneta huyo aliahidi kuendeleza kampeni za kumpeleka Bw Barasa nyumbani 2027 huku akiwarai wakazi wamuunge mkono Rais Ruto.
Katika eneobunge la Shinyalu, Bi Muhanda alizomewa na makundi ya vijana alipomwalika Rais Ruto awahutubie. Mbunge huyo mwakilishi wa kike alimwomba Rais azuru Hospitali ya Level 6 ya Kakamega kuona jinsi ambavyo wagonjwa walikuwa wakiteseka kutokana na huduma duni na ukosefu wa dawa.
Katika Kaunti ya Vihiga Gavana Wilbur Ottichilo, mbunge wa Luanda Dickson Maungu na Mbunge Mwakilishi wa Kike Beatrice Adagala walizomewa wakati wa kuzinduliwa kwa ujenzi wa soko jipya la Luanda.
Pia tofauti kati ya Bw Maungu na Spika wa Bunge la Kaunti ya Vihiga Chris Omulele ambaye alihudumu kama mbunge wa Luanda kati ya 2013-2022 zilidhihirika wazi. Bw Ottichilo alisema kuzomewa kwa viongozi kulichochewa na wapinzani wao wa kisiasa.
Katika Kaunti ya Bungoma, Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa na aliyekuwa Gavana Wycliffe Wangamati walijibizana mbele ya rais. Wawili hao wanaendeleza kampeni kali za kutwaa ugavana mnamo 2027.
Kule Busia, wafuasi wa Gavana Paul Otuoma waliwafurusha baadhi ya watu ambao walikuwa wameanza kumzomea mbele ya Rais Ruto kule Budalang’I. Watu hao walikuwa wafuasi wa mpinzani wake Vincent Sidai.
Leave a Reply