WABUNGE kutoka Kaunti ya Kakamega wameanzisha kampeni kali ya kuwashawashi Wakenya zaidi wajisajili kwenye Bima ya Afya ya Kijamii (SHA).
Hii ni licha ya malalamishi ya raia kuhusu changamoto mbalimbali ambazo wamekuwa wakipitia chini ya mpango huo ambao ulichukua nafasi ya NHIF.
Baadhi wamekuwa wakilalamika kuwa wamelemewa kujisajili kwenye SHA na wanaoenda hospitali wakighadhabishwa na hatua ya kutakiwa kulipia huduma za kimatibabu.
Akiwa kwenye ziara ya siku tano Magharibi mwa Kenya wiki jana, Rais Ruto alipigia debe bima hiyo mpya akisema kuwa inawajali na kuwajumuisha hata raia maskini.
“Lazima tushirikiane kuwasaidia Wakenya kunufaikia bima hiyo ya kimatibabu ili wapokee huduma nzuri,” akasema Rais Ruto.
Alisema yeye pamoja na wabunge walikuwa wakikatwa Sh27,000 kwenye mishahara yao ili kuwalipia wale ambao hawajiwezi ndipo wanufaikie bima hiyo ya SHA.
Rais alisema bima hiyo inalenga kuongeza idadi ya Wakenya ambao walikuwa wakinufaika chini ya NHIF kutoka milioni 10 hadi milioni 50.
Mbunge wa Mumias Magharibi Johnson Naicca na mwenzake wa Matungu Oscar Nabulindo wameanzisha kampeni kali maeneobunge yao kuwasajili wakazi kwenye SHA.
Akiwa ameandamana na wahudumu wa afya, Bw Naicca aliandaa mikutano minne kwenye wadi ya Mumias ya Kati, Etenje, Musanda na Nucleus kuwashaajisha wakazi wajisajili kwenye SHA.
“Wagonjwa wanaendelea kuteseka nyumbani kwa sababu hawawezi kupata matibabu. Kupitia SHA ambayo si pesa nyingi, kila Mkenya amehakikishiwa huduma bora za kimatibabu,” akasema Bw Naicca katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Musanda.
“Namwomba kila mtu ashiriki kwa kujisajili na SHA ili wasitatizike wakienda hospitalini,” akaongeza.
Bw Nabulindo ambaye aliwahutubia waumini kwenye Kanisa Katoliki la Ejinja alisema SHA itaimarisha uwezekano wa Wakenya wengi kupata matibabu hasa wale wenye mapato ya chini wakijumuishwa.
“SHA inazingatia na kutimiza mahitaji ya Wakenya wengi. Kinaya ni kuwa wanaonufaika ni watu kutoka Mlima Kenya ambao viongozi wao wanawahadaa Wakenya wengine kuwa SHA ni mbaya,” akasema
“Wale wanaowaambia SHA ni mbaya wanayataka maeneo yao wanufaikie bima hiyo huku nyinyi mkiachwa nyuma,” akaongeza.
Licha ya Kaunti ya Kakamega kuwa ya pili kwa wingi wa watu nchini, ni karibu watu 30,000 pekee wamejisajili kwa SHA huku ikiwa na watu milioni 1.8.
Leave a Reply