Wabunge kukutana kuweka mikakati ya muda uliosalia kabla ya 2027 – Taifa Leo


WABUNGE watakutana kujadili ajenda ya Bunge la Kitaifa kabla ya kurejelea vikao rasmi mwezi ujao, Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula alitangaza Alhamisi.

Mkutano utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu utajadili vipaumbele vya kisheria kabla ya bunge kurejelea vikao vyake rasmi Februari.

Bw  Wetang’ula alibainisha kuwa katika mkutano huo wabunge watajadili masuala ya katikati ya muhula wa Bunge  na  kutathmini utendakazi wa Bunge na kupanga jinsi ya kusonga mbele.

Akiwahutubia wabunge katika kikao maalum kilichofanyika Alhamisi, Januari 16, 2025, Spika Wetang’ula alitangaza kuwa kikao hicho kitafanyika mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru, kuanzia Januari 27 hadi 31.

Mkutano huu, unaofanyika katikati ya muhula wa Bunge la 13, utawapa Wabunge fursa ya kutafakari maendeleo yaliyopatikana katika vikao vitatu vya kwanza na kuweka mikakati ya ajenda za sheria kwa kikao cha nne kinachotarajiwa kuanza Februari, alieleza.

“Kikao hiki kitawawezesha Wabunge kutathmini mafanikio yaliyopatikana kufikia sasa na kujadili masuala muhimu ya kisheria yanayotarajiwa kuelekea mbele. Kufanyika kwake katikati ya muhula wa Bunge ni fursa ya kujiandaa kwa muda uliosalia wa muhula huu,” alieleza Bw Wetang’ula.

Programu ya kikao hicho itajumuisha mijadala ya pamoja na vipindi  vitakavyoongozwa na wataalamu wenye uzoefu, wakiwemo wabunge wa sasa na waliostaafu.

Wabunge wanatarajiwa kuchunguza maeneo ya kuboresha mchakato wa kisheria ili kuongeza ufanisi wa utawala na utoaji wa huduma.

Maandalizi ya mkutano huo yanaendelea, huku Karani wa Bunge la Kitaifa, Bw Samuel Njoroge, akitarajiwa kutoa maelezo ya kiufundi hivi karibuni.

Kikao  hicho maalum cha Alhamisi, kilichoitishwa kwa mujibu wa Kanuni ya Kudumu ya 29(3) na kutangazwa kupitia Notisi ya Kenya Gazette Na. 110 Januari 10, 2025, pia kilishuhudia  hatua kubwa za kutunga sheria.

 

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula. PICHA | MAKTABA

Ikumbukwe, Bunge la Kitaifa lilipitisha Mswada wa Watu Wenye Ulemavu, Mswada wa Seneti wa 2023.

Mswada huo, unaolenga kuoanganisha sheria za Kenya na Kifungu cha 54 cha Katiba, unaboresha haki na fursa kwa watu wanaoishi na ulemavu.

Kupitishwa kwa Mswada huo kunadhihirisha dhamira ya Bunge ya kukuza ushirikishaji na kulinda maslahi ya makundi yaliyo hatarini.

Mswada huo sasa unasubiri hatua ya kuidhinishwa rasmi kuwa sheria, jambo linalodhihirisha kujitolea kwa Bunge kushughulikia usawa wa kijamii.

Katika kikao hicho, Spika Wetang’ula, alitoa shukrani kwa msaada aliopokea kufuatia kifo cha mama yake, Mama Anna Nanyama Wetang’ula.

“Tuna shukrani kubwa kwa msaada mkubwa na usio na kifani mlionipatia katika kipindi hiki kigumu. Uwepo wenu na maneno yenu ya faraja, pamoja na yale ya Mheshimiwa Rais na wajumbe kutoka nchi jirani, yalionyesha kwa dhati mshikamano wa kweli,” alisema Spika.

 

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*