Wabunge wafufua ulafi wa kutaka waongezwe mshahara uliozimwa na Gen Z – Taifa Leo


WABUNGE  sasa wanashinikiza kutekelezwa kwa nyongeza ya mishahara ambayo ilisitishwa katika kilele cha maandamano ya vijana ya Juni 2024.

Wabunge hao walitumia Kikao Maalumu kilichoitishwa kuidhinisha watu saba walioteuliwa  katika Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) kushinikiza nyongeza ya mishahara.

Wabunge waliidhinisha uteuzi wa Sammy Chepkwony kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa SRC na wanachama Mej-Jenerali Mstaafu Martin Kizito Ong’onyi (aliyependekezwa na Baraza la Ulinzi); Mohamed Aden Abdi (aliyeteuliwa na Seneti kwa niaba ya kaunti); Jane Gatakaa Njage (aliyeteuliwa na Tume ya Utumishi wa Walimu); Dkt Gilda Odera (aliyeteuliwa na Shirikisho la Waajiri wa Kenya); Dkt Geoffrey Apollo Omondi (aliyeteuliwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi); na Leonid Ashihundu (aliyeteuliwa na Chama cha Mashirika ya Kitaalamu katika Afrika Mashariki).

Maandamano yaliyoongozwa na vijana, ambayo yalishuhudia vijana wakivamia Bunge kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya mnamo Juni 25, 2024, yaliwalazimisha wabunge kukataa mapendekezo ya nyongeza ya moja kwa moja ya mishahara yao.

Uasi ulioongozwa na Gen Z nchini kote ulimlazimu Rais William Ruto kuagiza kuchunguzwa upya kwa mpango wa wabunge kuongezwa mishahara kufuatia malalamiko ya umma.

Maandamano hayo makubwa pia yalimlazimu Dkt Ruto kutupilia mbali Mswada tata wa Fedha wa 2024 ambao ulijumuisha nyongeza ya ushuru.

Kufuatia maandamano hayo, mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich pia alilazimika “kuzima” nyongeza ya mishahara ya maafisa wa Serikali kutokana na alichoita “hali halisi ya sasa ya uchumi.”

Awali SRC ilikuwa imependekeza nyongeza ya mishahara ya kati ya asilimia mbili hadi tano kwa maafisa wote wa serikali, wakiwemo majaji na wabunge.

Wabunge na Maseneta, ambao mshahara wao ni Sh725,502 ungeongezwa hadi Sh739,600 kila mwezi kama uasi wa Gen-Z haungefanyika Juni 2024. Wabunge wa Kenya ni baadhi ya wanaolipwa zaidi duniani.

Wabunge waliochangia mjadala wa kuidhinishwa kwa watu saba walioteuliwa kuhudumu katika SRC waliwataka makamishna wapya kuoanisha mishahara yote ya utumishi wa umma na wala si kulenga tu malipo na marupurupu ya wabunge.

 

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah

“Wabunge kama Wakenya wengine wanastahili nyongeza ya mishahara,” Kiongozi wa Wengi Bw Kimani Ichung’wah alisema.

Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed alisema kuna dhana potofu katika SRC kwamba iliundwa kushughulikia mishahara ya wanasiasa.

Alidai kuwa tume hiyo mpya inapaswa kuanza kwa mpangilio mpya na kuangalia mswada wa mishahara ya umma kikamilifu na kuioanisha.

“Lakini utaona 2027, tume itakuwa ikichapisha notisi zinazosema mishahara ya wabunge ipunguzwe,” Bw Mohamed, Mbunge wa Suna Mashariki, alisema.

“Msichapishe mishahara kwenye gazeti la serikali kwa nia mbaya. Fanyeni mapema ili watu wanaotaka kuwa wabunge waamue wanataka kuendelea au la. Acheni mishahara yetu…Tunalipa karo za shule, tunachangia harusi, mazishi, na masuala mengine ya kijamii. SRC inadhani sisi ni kundi la wacheshi tu…watu wasio na maana.”

Mbunge wa Rarieda Otiende Amolo aliambia SRC mpya kuzingatia kazi ambayo mbunge hufanya na wala sio sifa za chini kabisa katika kuweka mishahara yao.

Waandamanaji kwenye barabara ya Kenyatta Avenue mjini Nairobi kupinga Mswada wa Fedha 2024 na uongozi mbaya nchini, mnamo Juni 25, 2024. PICHA | BONFACE BOGITA

“Gen Z walitusukuma kukataa nyongeza ya mishahara ambayo ingeanza kutumika Julai, 2024 wakati tulihitaji nyongeza. Ilibidi turudi kwa wapiga kura wetu kusema tunakataa nyongeza ya mishahara,” Zamzam Mohamed, Mwakilishi wa Wanawake wa Mombasa alisema.

“Mishahara tunayopata inaenda kwa jamii tunazohudumia … tunashambuliwa bado tunaporudi nyumbani, tunalemewa na maombi mengi ya kifedha kama vile basari, bili za hospitali,na mazishi. Tunatumia pesa zote tunazopata hapa kwa watu wanaotuchafua.”

Bi Mohamed alisema amekuwa maskini zaidi kwa sababu ya kutoa kidogo anachopata kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wapiga kura wake.

“Ninataka kutoa wito kwa Wakenya kuunga mkono nyongeza ya mishahara kwa Wabunge. Ikiwa tutapata nyongeza ya mishahara, tafadhali tuunge mkono.”

Mbunge wa Nyeri Mjini Duncan Mathenge aliitaka SRC mpya kuhakikisha watu walioajiriwa wanaishi maisha yanayostahili.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*