Wabunge wataka afisa wa KWS aliyepiga risasi mkazi kwa kuingia mbuga ya Tsavo akamatwe – Taifa Leo


MUUNGANO wa wabunge wa Pwani (CPG) umemtaka Mkurugenzi mkuu wa Huduma za Wanyama nchini kujiuzulu iwapo hatamchukulia hatua afisa wa KWS aliyempiga risasi mkazi mmoja huko Garsen kaunti ya Tana River kwa misingi ya kuingia katika mbuga ya Tsavo Mashariki bila ruhusa.

Wakizungumza baada ya kuwasilisha matakwa yao katika afisi za KWS ukanda wa Pwani, walitaka hatua ichukuliwe dhidi ya maafisa hao ndani ya siku saba ambao kwa mujibu wao, walitumia nguvu kupita kiasi kupambana na visa vya kuingia mbugani.

Mkazi wa eneo hilo Bw Mohammed Juge ambaye pia ni mtetezi wa haki alieleza kuwa, mwendazake Bw Isak Jarso, aliuawa akiwa nyumbani kwake, kisa kinachoibua maswali kuhusu sababu za kuuawa kwake.

“Jamii ya Wafugaji wa Orma wameishi katika eneo hilo hata kabaa ya 1948 mbuga hiyo ilipochapishwa katika gazeti rasmi la serikali kama mbuga ya Wanyama. Iweje binadamu apigwe risasi kwa kuingia tu kwenye mbuga hiyo kutafuta malisho au maji ya mifugo wake? Hata Ndovu akipita yuapigwa tu sindano ya kulala,” akasema Bw Juge.

Kwa mujibu wa mbunge wa eneo la Garsen ambako tukio hilo lilitokea Ali Wario, Bw Jarso alikuwa mpenda watu na mtu wa dini.

Aliuliza mbona uchunguzi wa mauaji hayo umechukua zaidi ya wiki moja licha ya bunduki za maafisa wa KWS kuwaslilishwa kwa DCI na hakuna aliyekamatwa kuhusiana na mauaji hayo.

“Mimi hapa namfikiria yule mzee na familia yake ambayo sasa imebaki bila baba. Hadi wa leo hakuna lolote lililofanyika. Iwapo huyu Mkuregenzi mkuu wa KWS hawezi kuwachunga maafisa wa KWS badi naye ajiuzulu,” akasema Bw Wario.

Aliongeza kuwa, Rais William Ruto alikuwa ametoa amri ya KWS kutengeneza njia ili wakazi watumie kupita wanapoendelea na shughuli zao ili kupunguza mizozo ya maafisa hao na wakazi. Licha ya amri hiyo kutolewa hakuna lililofanyika.

Mbunge wa Matuga Kassim Tandaza alihoji kuwa, tatizo kubwa lilikuwa rasilmali haswa maji na kulipaswa kuwa na njia ya kuwaondoa wananchi katika mbuga bila kutumia nguvu kupita kiasi.

“Tunataka hatua ichukuliwe ndani ya siku saba kwa kuwa tukirejea hapa huenda hatua tutakayorudi nayo itakuwa moja ambayo haitafurahisha. Ila matakwa yetu kwa ajili ya watu wetu tumeyawasilisha,” akasema Bw Tandaza.

Seneta wa Mombasa Mohamed Faki na mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba ambao pia walikuwa wameandamana na viongozi hao, walimtetea Bw Wario dhidi ya madai kuwa alikuwa akiwachochea wananchi.

“Wamekuwa wakimtishia Bw Wario asizungumzie swala hili lakini, yeye kama mbunge lazima atetee watu wake. Kazi ya mbunge ni kudhibiti utendakazi wa serikali,” akasema Bw Faki.

Afisa wa KWS aliyepokea barua hiyo kwa niaba ya KWS, Vincent Ongwaye ambaye ni Msimamizi mkuu wa hifadhi alieleza kuwa barua hiyo ingeshughulikiwa ili kuleta amani kati ya jamii na huduma hiyo.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*