KAMATI ya bunge imetoa wito kwa Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali, Nancy Gathungu, kufanyia uchunguzi wa kina mfumo wa bili za stima wa kampuni ya Kenya Power kufuatia malalamishi kutoka kwa wateja kuhusu bili za juu kupindukia.
Katika ripoti yake kuhusu kiini cha bei ya juu ya stima, Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Nishati, inamtaka Bi Gathungu kubaini iwapo kuna udanganyifu, ufisadi au aina nyingine ya utapeli katika mtindo unaotumiwa kuhesabu bei ya stima na kampuni hiyo.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mwala, Vincent Musyoka vilevile inamtaka Bi Gathungu kupitia ukaguzi wake, kubaini ada za bili za stima zinazotozwa na KPLC kwa wateja wote wanaolipa kabla na baada ya matumizi.
“Kwamba katika muda wa miezi sita kufuatia kuidhinishwa kwa ripoti hii, na kwa kuambatana na vipengee 37 na 39 vya Sheria kuhusu Ukaguzi wa Hesabu za Umma 2015, Mkaguzi Mkuu atafanyia KPLC ukaguzi wa kina utakaojumuisha michakato ya ununuzi na kutoa kandarasi, mifumo ya bili na kukusanya mapato, usimamizi wa wafanyakazi na mishahara, usimamizi wa madeni, na utendakazi, na kuwasilisha ripoti kwa bunge la kitaifa,” inasema ripoti.
Wakati wa udadisi huo, KPLC iliangaziwa na kamati na wadau waliowasilisha maoni yao kwa wabunge huku idadi kubwa wakishutumu kampuni hiyo kuwa moja kati ya vizingiti vinavyozuia kudhibiti gharama ya juu ya umeme nchini.
Ikitoa mawasilisho yake mbele ya Kamati Agosti, afisi ya Mkaguzi Mkuu aliyewakilishwa na Naibu Jenerali Stanley Mwangi, aliwashangaza wabunge aliposema wateja wanalipia bili ambazo hawakutumia na ada wanazolimbikiziwa na KPLC haziwezi kufuatiliwa.
Kuhusu uzalishaji, upitishaji na usambazaji umeme, mkaguzi mkuu alieleza kamati kwamba kuna dosari kwenye hesabu za hasara hali inayotokana na ripoti za uchunguzi zilizopitwa na wakati, vipimo vinavyegemea upande mmoja na makosa ya kihesabu.
Bw Mwangi alieleza wabunge kuwa wamegundua kuwepo vipimo vya matumizi ya umeme (mita) vipimo vilivyo na walakini na makosa kati ya mita za kukagua na mita kuu hali ambayo imesababisha wateja kupatiwa bili zisizoambatana na mita zao.
Alisema miongoni mwa viwanda 96 vinavyozalisha umeme kwa Kenya Power, ni 38 pekee vilivyo na mita za kukagua.
Cha kustaajabisha zaidi ni kuwa mita zote 38 hazikuwa zimeunganishwa na kituo kikuu cha kusambazia umeme.
“Karibu asilimia 20 ya bili za wateja haziwezi zikalinganishwa na kiwango halisi cha matumizi wala kampuni inayosambaza stima kuihusisha na mteja fulani,” alisema mkaguzi.
“Ingawa usimamizi umeashiria kwamba wamekuwa wakijitahidi kupunguza hasara ya stima, hakuna ushahidi kuhusu juhudi na ufanisi uliofanyika katika kuboresha masuala haya. Kulipisha hasara kunaathiri bei ya stima.”
Imetafsiriwa na Mary Wangari
Leave a Reply