MAMIA ya wafanyabiashara Jumapili waliandamana kulalalamikia ukosefu wa soko la kisasa kwenye mji wa Kiriari, Kaunti ya Embu.
Wafanyabiashara hao walishutumu serikali ya Kaunti ya Embu kwa kuchukua muda mrefu kuwajengea soko la kisasa.
“Tuliahidiwa na serikali ya kaunti kuwa tungejengewa soko la kisasa Septemba mwaka jana. Hata hivyo, hadi leo, ujenzi huo haujaanza licha ya kuwa tumelipa ada zote za kufanya biashara,” akasema Rose Gitavi.
Wakiongozwa na Askofu Joseph Weru, wafanyabiashara hao walisema wameteseka kwa kipindi kirefu na serikali ya kaunti inastahili kuchukulia suala hilo kwa uzito.
“Tumekuwa tukiuza bidhaa zetu kando ya barabara na kuhatarisha maisha yetu. Bidhaa zetu na mazao kama kabeji, nyanya, viazi na maharagwe huwa zimefunikwa kwa vumbi na kusababisha tuwapoteze wateja,” akasema Askofu Weru.
“Kama wafanyabiashara hatuna furaha na tunataka utawala wa kaunti ushughulikie suala hili mara moja,” akasema Askofu Weru. Walisema ni wajibu wa serikali ya Gavana Cecily Mbarire kutoa mazingira mazuri ya kufanyia biashara.
“Hii serikali ya kaunti inastahili kuonyesha kuwa inawajali wafanyabiashara ambao wanachangia ukuuaji wa kiuchumi wa kaunti,” akasema Askofu Weru.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Michael Maina, alisema kaunti ilikuwa inunue ardhi ya kujenga soko mwaka jana lakini hakuna chochote ambacho kimefanyika.
“Tunaendelea kuchoka kusuburi soko la kisasa,” akasema Bw Maina. Wafanyabiashara hao walitishia kuwa watakataa kulipa ada iwapo malalamishi yao hayatashughulikiwa.
Leave a Reply