Wafanyakazi shule ya Kijamii ya Gatoto, Embakasi wahofia hatima yao – Taifa Leo


WAFANYAKAZI 43 katika shule ya jamii ya Gatoto eneo la Mukuru kwa Reuben, Embakasi Kusini wamebaki katika hali ya sintofahamu kuhusu hatma yao baada ya wasimamizi wa awali chini ya mpango wa Gatoto Intergrated Development Programme kuondolewa.

Mfanyakazi mmoja ambaye hakutaka kutajwa alisema kuna wasiwasi mkubwa kuhusu mishahara yao. Alisema walimu waliosajiliwa na TSC walifanya mkutano na mwalimu mkuu mpya na kuonywa dhidi ya kufanya maamuzi ya haraka ya kujiuzulu.

“Hadi sasa, hatujui ni nani atatulipa, ingawa uongozi mpya umetuhakikishia. Ninajiuliza tu jinsi na lini nitapata mshahara wangu,” alisema mfanyakazi huyo.

Baadhi ya wazazi na wakazi wakiandamana kupinga kugeuza shule hiyo na kuwa ya umma. Picha|Fridah Okachi

Mfanyakazi huyo alisema wasiwasi uliongezeka zaidi baada ya walimu watano kutumwa na TSC.

“Walimu wawili tayari wameondoka bila hata kuwasilisha barua za kujiuzulu. Wengine wengi wanazingatia kuondoka,” aliongeza mfanyakazi mwingine.

Suala lingine linaloisumbua shule ni ukosefu wa chakula cha kutosha kwa walimu na wanafunzi. Alibainisha mabadiliko makubwa ambayo yamewalazimisha walimu na wanafunzi kutegemea mgao mdogo wa chakula, ambao huenda ukaisha hivi karibuni.

Hii ikitokana na magunia 50 ya mahindi yaliyosalia.

“Sasa hakuna kiamsha kinywa kwa walimu na wanafunzi. Tunapata tu uji saa nne asubuhi na sehemu ndogo ya chakula aina ya githeri mchana,” alilalamika mfanyakazi huyo.

Mabadiliko hayo yanaathiri wazazi na wanafunzi ambao walikuwa wakinufaika na ufadhili wa elimu chini ya GIDP.

Ruth Ndunge, mama wa watoto sita, alieleza huzuni yake kuhusu jinsi ya kusomesha wanawe watatu ambao wako shule za sekondari.

Alifichua watatu hao, walilipiwa karo baada ya kufanya vizuri katika mitihani yao ya shule ya msingi.

Bango katika shule ya Jamii ya Gatoto, mtaa wa Mukuru. Picha|Fridah Okachi

“Watoto wangu hawajarudi shule kwa sababu hakuna mtu wa kulipa karo yao. Unaponiona nikilia, ni kwa sababu nimezidiwa na wasiwasi,” alitirirkwa kwa machozi.

Mfaidi mwingine ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Maseno Bw Victor Achula. Bw Achula alilaumu hatua ya serikali ya kuchukua shule hiyo, akisema inaweza kuathiri ufadhili wa masomo yake.

“Huu ni mwaka wangu wa tatu chuoni, lakini sasa sijui itakuwaje kwani waliokuwa wakilipa karo yangu tayari wamejiondoa,” alisema.

Mwenyekiti wa bodi GIDP Bw Felix Mwangangi, alikosoa Wizara ya Elimu kufanya mabadiliko hayo bila kuwahusisha.

“Wizara ya Elimu haikutuma mawasiliano rasmi kuhusu kuifanya shule kuwa taasisi ya umma. Shule kwa sasa ina wanafunzi 1,000, na akiba ya chakula kitadumu kwa wiki mbili pekee,” alisema.

Lango kuu la Shule ya Jamii ya Gatoto, mtaa wa Mukuru, Embakasi Kusini, Januari 9, 2025. Picha|Fridah Okachi

Taifa Dijitali ilithibitisha kuwa shughuli za masomo zinaendelea kama kawaida chini ya uongozi mpya wa mwalimu mkuu Margret Kimani, ambaye anadai alitumwa na Tume ya Huduma za Walimu (TSC).

Bi Kimani, aliyekataa kuzungumza zaidi, alisema shule iko imara.

Chifu wa eneo hilo, Bw David Ndirangu, aliyempokea mwalimu mkuu mpya, alithibitisha kuwa shule sasa iko chini ya udhibiti wa serikali.

“Kuna utawala mpya, na mambo bado yanatulia. Ninavyojua, serikali imetuma walimu saba. Serikali haiwezi kutoa fedha kwa miradi ya kibinafsi, kwa hivyo mwalimu mkuu mpya ameanza shughuli ya kufungua akaunti mpya,” alisema.

Hata hivyo, Afisa wa Elimu wa Kaunti Ndogo ya Embakasi Kusini, Bi Mary Kimeu, alikataa kutoa maoni.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*