Wagonjwa wa upasuaji wakodolea kifo mfumo wa SHIF ukikwama – Taifa Leo


WAGONJWA wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa dharura kuokoa maisha yao wamekuwa wakicheleweshwa kwa muda mrefu kwani hospitali kote nchini zinasubiri mfumo wa Hazina ya Afya ya Jamii (SHIF) kuboreshwa.

Kwa takriban wiki moja, Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) inayosimamia Shif haijatoa idhini inayohitajika ili hospitali zifanyie wagonjwa upasuaji.

Hali hii imewaacha wagonjwa hao wakiteseka kimya kimya.

Tovuti ya uidhinishaji ya SHA iliundwa ili kurahisisha uidhinishaji wa upasuaji na taratibu nyingine za matibabu, lakini badala yake, mfumo huo umegeuka kuwa kizuizi.

Kwa wiki moja, tovuti hiyo haijawa ikifanya kazi, na kusababisha ucheleweshaji mkubwa wa upasuaji unaopangwa na wa dharura. Katika hospitali moja mjini Kitale, wafanyakazi waliripoti kukosa kupata idhini ya SHA kuhudumia wagonjwa 10 wanaohitaji upasuaji mwishoni mwa Novemba.

“Ilibidi tuwarudishe wagonjwa nyumbani, tukiahidi kupanga upasuaji wao mara tu idhini itakapopatikana,” msimamizi wa hospitali hiyo aliambia Taifa Leo.

Ucheleweshaji una matokeo mabaya

“Ucheleweshaji huu una matokeo mabaya. Baadhi ya visa hivi vinahitaji kushughulikiwa haraka, lakini hatuwezi kubeba gharama bila idhini.”

Katika visa vya dharura, hospitali sasa zinawataka wagonjwa kulipa pesa taslimu kwanza.

“Hatuna chaguo. Kufanya upasuaji bila kibali kunamaanisha kwamba tunajiweka katika hatari ya kutolipwa. Kwa sasa, malipo ya pesa taslimu ndiyo njia pekee ya kuendelea na upasuaji wa visa vya dharura,” msimamizi mwingine wa hospitali alisema.

Dkt Brian Lishenga, Mwenyekiti wa Kitaifa wa Chama cha Hospitali za Kibinafsi alisema tatizo hili linatokana na tovuti ya uidhinishaji ya SHA.

Mabadiliko hayo yalianzisha sheria mpya zinazohitaji maombi yote ya uidhinishaji kabla ya huduma za upasuaji kuthibitishwa na mkaguzi ndani ya mfumo.

“Hapo awali, mchakato wa kuidhinisha kabla ya huduma haukuwa na mkanganyiko,” Dkt Lishenga alieleza.

“Lakini inaonekana kulikuwa na dosari katika mfumo huo ulipozinduliwa miezi miwili iliyopita. Takriban kila utaratibu ulikuwa unaidhinishwa moja kwa moja. Hii ilisababisha kuongezeka kwa madai ya ada za upasuaji, ambazo zimepanda na kufikia karibu Sh5 bilioni ambazo hazijalipwa ndani ya mwezi mmoja. Wasiwasi ulizuka kwamba hali hii haikuwa endelevu kifedha na kusababisha marekebisho.”

Upasuaji ambao kwa kawaida hupangwa mapema, umecheleweshwa kwa muda usiojulikana huku hospitali zikisita kufanya wa dharura kwa hofu ya kujilimbikizia madeni kisha zikose kulipwa na SHA.

Mgonjwa aliyepata ajali mbaya

“Mwishoni mwa juma, tulipokea rufaa ya mgonjwa aliyepata ajali mbaya, alihitaji kufanyiwa upasuaji ambao ulipaswa kufanyika jana, lakini bila idhini, mgonjwa ameachwa na maumivu makali. Isipokuwa kwa huruma tu, hakuna tunachoweza kufanya na atalazimika kungoja,” alisema.

“Kwa sasa nina visa saba vinavyongoja kuidhinishwa kwanza,” alisema daktari ambaye hakutaka jina lake litajwe.

“Ikiwa nitafanya bila idhini, basi nitabaki na gharama. Bado ninadai Hazina ya Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) pesa nilizofanya upasuaji.

“Nilipata funzo na sitarudia kosa hilo tena,” Dk Lishenga alisema.

“Wagonjwa wanaotegemea bima ya kibinafsi wanakabiliwa na vikwazo zaidi. Bila SHA kuidhinisha, kadi zao za bima hazitumiki. ‘Hii inaleta ugumu zaidi kwa wagonjwa ambao walidhani walikuwa na usalama wa kifedha,” alibainisha Dk Lishenga. Dkt Lishenga alisema amezungumza suala hilo na Mwenyekiti wa SHA, Dkt Ali Muhammed.

Kulingana na Dkt Muhammed, wasiwasi kuhusu ufanisi wa idara ya uidhinishaji ulisababisha marekebisho kamili ya mfumo.

Lakini kwa wagonjwa kama wale wanaosubiri Kitale na kote nchini, kila siku inayopita bila hatua kuchukuliwa, huleta mateso yasiyostahimilika.

Mgogoro huo umefichua udhaifu wa mfumo wa huduma za afya, huku Wakenya walio hatarini wakibeba mzigo mkubwa wa uzembe wa wahusika.

Juhudi za kumpata mwenyekiti wa SHA

Juhudi za kumpata mwenyekiti wa SHA, Dkt Ali hazikufua dafu kwani hakujibu simu na jumbe tulizomtumia.

“Mwanzoni mwa mfumo wa SHA, nilikumbana na changamoto kubwa,” akasimulia Dkt Ruto Cheregany.

“Mgonjwa alikuja na ujauzito uliohitaji upasuaji wa dharura. Tulimkimbiza moja kwa moja kwenye chumba cha upasuaji. Baada ya upasuaji, tuliwasilisha ombi kuidhinishwa, lakini lilikataliwa,” alisema.

Dkt Cheregany alibainisha kuwa mahitaji hayo magumu huacha wataalamu wa matibabu katika hali ngumu.

“Katika hali kama hizi, inakuwa vigumu kuweka kipaumbele kwa taratibu za kuokoa maisha bila idhini. Njia mbadala ni kuwauliza wagonjwa walipe pesa taslimu kabla ya kuhudumiwa, ambazo si wote wanaweza kumudu,” alisema, akisisitiza matatizo yanayowakabili madaktari na wagonjwa.

Wataalamu wa afya wanahimiza hatua za haraka zichukuliwe ili kuokoa SHA na kuzuia kuporomoka kwa jumla kwa mfumo wa ufadhili wa huduma za afya.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*