KIFO cha mwanabiashara Jacob Juma Mei 6, 2016 kilipisha mgogoro wa umiliki wa nyumba mojawapo iliyoko Westlands, kati ya wajane wawili Miriam Wairimu na Lydia Tabuke.
Bi Tabuke analalamikia ukosefu wa ajira na kuwa ameshindwa kulipa kodi ya nyumba anayoishi eneo la Ngong, Kaunti ya Kajiado.
“Mimi ninafaa kuishi hapa Westlands sababu Wairimu na watoto wake wawili wanaishi Karen,” aliteta katika mahojiano na Taifa Leo.
Juhudi za Bi Tabuke kuhamia Westlands Jumatano Novemba, 11 2024 ziligonga mwamba baada ya vitu vyake kudaiwa kutupwa nje usiku huo na mjane mwenza.
“Mimi sijamfurusha yeyote (Tabuke) kutoka kwa nyumba hii. Kilichofanyika ni kuwa alivunja lango na kuharibu vitu hapa. Ni mimi nimekuwa nikitunza nyumba hii kwa kulipa wafanyakazi na ada za maji na umeme,” akajibu Bi Wairimu.
“Kuna haja gani mimi na watoto wangu tulale nje na hali tuna nyumba hii hapa ambayo hakuna anayeishi ndani?” akauliza Bi Tabuke.
Kesi kortini
Stakabadhi za korti zinaonyesha kuwa Bi Wairimu amekuwa akipigania umiliki wa nyumba inayozozaniwa kortini tangu ahame 2011.
Nyaraka za mahakama zimenakili mwanamke mwingine Bi Jane Wanja amekuwa akidai mali hii na kuishi hapa.
Bi Wairimu aliambia Taifa Leo ameishi katika nyumba hiyo kwa miaka mingi na alipata watoto wake wawili nyumbani humo.
Bi Wanja alidai marehemu alimkopa Sh 5 milioni; pesa ambazo anasema hajalipwa.
Mahakama iliamua kinyume na matarajio ya Bi Wanja mnamo Agosti 2024 na kwa hivyo nyumba inayopiganiwa ikabaki bila mkazi.
“Mbona Bi Tabuke asiwe na subira ya uamuzi wa korti Februari 2025 ili tubaini njia ya kurithi mali?” akauliza Bi Wairimu.
Wajane hawa wawili wanatambulika katika stakabadhi za mahakama kuwa wajane wa Jacob Juma.
Bi Wairimu analalamika akimtuhumu Bi Tabuke kwa kukaa mbali wakati kesi ya nyumba hiyo ilikuwa inaendelea.
Anadai kuwa Bi Tabuke aliibuka tu baada ya Bi Wanja kuondolewa kutoka katika makazi hayo na amri ya mahakama.
Kifo cha Juma
Bw Juma aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya gari lake mwaka wa 2016.
Hakuna kilichoibwa katika ufyatuaji huo wa usiku ambao ulikita matundu ya risasi angalau kumi kwenye gari hilo.
Simu na pesa zilipatikana garini humo.
Bw Juma alikuwa mwanakandarasi ambaye pia alihusika katika sekta ya uchimbaji madini.
Wajane hawa wawili – Tabuke na Wairimu – wana watoto wawili kila mmoja.
Inadaiwa kuna wanawake wengine waliokuwa na uhusiano na Bw Juma lakini wamedinda kuhusishwa na umiliki wa mali iliyoachwa na marehemu kwa sababu wako katika ndoa nyingine.
Leave a Reply