
MPANGO wa kuwatafutia vijana kazi katika mataifa ya nje almaarufu kazi majuu, wafika eneo bunge la Dagoretti Kusini, baada ya mbunge wa eneo hilo Bw John KJ Kiarie kuandaa hafla ya vijana kujiandikisha katika uwanja wa Taasisi ya Ufundi ya Kinyanjui.
Kulingana na mbunge huyo, alishirikiana na Katibu Mkuu wa Masuala ya Ughaibuni Roseline Njogu ili kuunganisha vijana wenye talanta na kazi katika mataifa mengine. KJ alisisitiza umuhimu wa wakazi wa Dagoretti kujitolea kujielimisha kuhusu ajira zinazopatikana katika nchi nyingine.
KJ aliwasuta baadhi ya wanasiasa aliodai hutoa tetesi kwamba mpango huo si mzuri.
“Kazi kwa ground hii Dagoreti yetu, ukienda pale kuanzia Junction, ufuate Ngong road hadi ufike kule Karen utaona pande zote mbili za barabara zimejaa fundi na seremala ambao wanauza vitu mbalimbali,” alisema mbunge huyo.
“Kuna tetesi ambazo utasikia na wengine kuhusu Kazi Majuu, wanatueleza kwamba huenda sio jambo zuri tutume watu wetu nje. Huyo ambaye anaeneza tetesi hizo huenda akapungukiwa na ujumbe au ufahamu,” aliongeza.

Baadhi ya vijana waliohudhuria hafla hiyo walisema wana matumaini ya kupata kazi hizo ambazo zina malipo mazuri. Bw Brian Mwashi, 32, alisema kuwa amekosa kazi kwa muda mrefu ambayo inachangia kuzima ndoto yake.
“Nimefika hapa kuangalia ni kazi zipi ambazo zinatolewa ili nijiunge na kunufaika. Kwangu binafsi nimekuwa nikitafuta ajira nchini na imekuwa ngumu kwangu. Ndoto zangu za kuwa na maisha bora zimedidimia kutokana na mapato madogo,” alieleza Bw Mwashi.
Wakati uo huo, Bi Roseline Njogu aliwashauri viongozi kuchukua hatua zaidi kuelimisha umma kuhusu kasumba inayoenezwa kuwa serikali haiwaajiri vijana bali kuwasafirisha nje ya nchi.
“Kitu kingine naomba wabunge waweze kueleza umma kuhusu ajira za nje hadi watakapoelewa ajira za nje na serikali basi dhana kuwa serikali haiwezi kutafutia wananchi ajira itaisha. Wengi hufikiria tunawatafutia ajira ambazo zina malipo madogo na kuteseka lakini si hivyo,” alieleza Bi Njogu.
Kwa sasa Wizara ya Mashauri ya Kigeni inatafuta mbinu ya kushirikiana na taasisi za kiufundi ili kuanza mpango wa masomo ambao utawezesha vijana wengi kupata ajira.
“Hapa mitaani kuna wale ambao tunawaita mtu wa bucha, lakini yule mtu anakata nyama ndio anatazamiwa na watu wengi,” alikamilisha Bi Njogu.
Leave a Reply