Wakazi Shimba Hills walilia lami miaka 61 baada ya uhuru – Taifa Leo


HUKU taifa likiadhimisha Sikukuu ya Jamhuri, wakazi wa Shimba Hills, Kaunti ya Kwale, wanahisi kusahauliwa kimaendeleo kwa kukosa barabara ya lami.

Barabara ya Mrima–Mwabungo yenye urefu wa kilomita 56 ni ya mchanga na inaunganisha Shimba Hills na Barabara Kuu ya Likoni-Lungalunga.

Hata hivyo, hali mbaya ya barabara hiyo hasa msimu wa mvua imekuwa changamoto kwa wakazi ambao usafiri wao unaathirika pakubwa kwani haiwezi kupitika.

“Barabara hii imekuwa ahadi ya kisiasa kwa miaka mingi. Wanasiasa huahidi kuitengeneza kila uchaguzi, lakini baada ya kupigiwa kura, sisi husahaulika,” alisema Boaz Mwakasimu, Katibu wa Wakazi wa Shimba Hills.

Akizungumza na Taifa Leo, alielezea kuwa mara nyingi magari ya kubeba bidhaa kama vile matunda, ambulensi, na hata bodaboda, hushindwa kupita kutokana na matope na mashimo makubwa.

Shimba Hills, ambayo sasa ni kaunti ndogo, ni eneo la ukulima Kwale, huku matunda na mimea mingine ikipandwa na kuuzwa kwa wakazi katika miji kama vile Ukunda.

Rhoda Matheka, mfanyabiashara wa eneo hilo, alisema hakuna magari ya usafiri wa umma yanayopita barabara hiyo.

“Lazima utumie bodaboda ambayo inatoza hadi Sh500 kufika Ukunda. Mvua ikinyesha, hatuwezi hata kupata bidhaa tunazouza,” alisema.

Kwa upande wake, Richard Sitoti alilalamika kuwa hali ya barabara imekuwa kikwazo kikuu kwa maendeleo.

“Tumepata kiwanda cha kutengeza sharubati kutokana na matunda mbalimbali, lakini hali ya barabara itafanya iwe vigumu kusafirisha matunda hayo kufika kiwandani,” alisema Bw Sitoti, ambaye pia ni mkulima.

Mbali na kilimo, huduma muhimu kama vile afya na elimu zimeathiriwa vibaya na hali mbovu ya barabara.

Wakazi wanasema kuwa kufikia huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Msambweni pia ni changamoto kubwa, hasa wakati kuna dharura.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*