Wakazi wa Kisumu walia mafuriko mradi ukiendelea kucheleweshwa – Taifa Leo


MAELFU ya wakazi wa Kaunti za Kisumu na Kericho, sasa wanashutumu serikali kwa kuchelewesha ujenzi wa bwawa la Koru Soin wanaosema lingewasaidia wakati huu wa mafuriko.

Mpango wa ujenzi wa bwawa hilo uliwapa matumaini sio tu ya kutatua tishio la kudumu dhidi ya mafuriko bali pia kuwafanya wasahau uhalifu na kifo cha waziri wa zamani Dkt Robert Ouko ambaye mwili wake ulipatikana katika eneo la Got Alila, Koru, Kaunti Ndogo ya Muhoroni.

Hata hivyo, matumaini yao sasa yanaendelea kudidimia kwani miaka 34 baadaye, mradi huo haujawahi kuendelezwa.Hali hiyo sasa imewaathiri pakubwa wakazi ambao wamelazimika kuhama makazi yao kutokana na mvua inayoendelea kunyesha katika sehemu mbalimbali za nchi.

Kufikia Jumanne wiki hii, Katibu katika wizara ya Usalama wa Ndani Dkt Raymond Omollo, alitangaza kwamba mafuriko ambayo yameshuhudiwa katika wiki mbili zilizopita yamesababisha vifo vya watu 12, na kuwafanya mamia kuhama makazi yao.

Kando na athari hizo, Dkt Omollo alisema kuwa mwili wa mtu mmoja ambaye alisombwa na maji hayo bado haujapatikana.Familia zaidi ya 300 ziliathiriwa katika kijiji cha Nyadina, Nyakach, zikifurushwa makwao baada ya Mto Sondu Miriu, kuvunja kingo zake kufuatia mvua kubwa iliyonyesha usiku kucha.

Dkt Omollo pia alidokeza kuwa zaidi ya kaunti 20 zimeathiriwa, huku Kisumu ikiwa ndiyo iliyoathiriwa zaidi.Katika Kaunti Ndogo ya Bunyala, Dkt Omollo alitembelea Shule ya Msingi ya Lunyofu, ambayo kwa sasa inahifadhi familia 500 zilizohamishwa.

Alisimamia usambazaji wa chakula na bidhaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mchele, maharagwe, blanketi, na vifaa vya matibabu, akisisitiza dhamira ya serikali ya kuhakikisha kuwa walioathiriwa wako salama.

Kando na hayo, alisema kwamba zaidi ya familia 3,000 Busia zimeathiriwa na mafuriko huku akisisitiza kuwa walio katika maeneo hatari wahamie maeneo salama.

Pia alitangaza mipango ya uendelezaji wa miundombinu, ikiwa ni pamoja na upanuzi wa barabara na ujenzi wa bwawa la juu ambalo ni Kilomita 4-5 ili kudhibiti mtiririko wa maji.

Maadhara ya mafuriko Nyando yamechangiwa na ukosefu wa suluhu ya kudumu ambayo ni pamoja na ujenzi wa bwawa hilo.

Taifa Leo ilipotembelea eneo hilo mwishoni mwa mwaka jana, wakandarasi wawili, China Jiangxi International Kenya Limited na China Jiangxi International Economic and Cooperation Company Ltd walikuwa wameanza kupeleka vifaa vya ujenzi katika eneo ambao ujenzi ulifaa kufanyika.

IMETAFSIRIWA NA WINNIE ONYANDO



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*