Wakazi wataka wasafishiwe mazingira baada ya wanajeshi wakimbizi kutoka Somalia kuenda haja kiholela – Taifa Leo


WAKAZI wa Ishakani mpakani mwa Kenya na Somalia wanaililia serikali na wahisani kuwasaidia kukarabati miundomsingi na mazingira yaliyochafuliwa baada ya kijiji hicho kusitiri wanajeshi wakimbizi kutoka nchi jirani ya Somalia.

Majuma mawili yaliyopita, Ishakani, ambacho ni kijiji kisichojulikana kutokana na hadhi yake ya chini, kiligeuzwa kuwa kambi ya maafisa zaidi ya 900 wakimbizi wa kijeshi kutoka Somalia.

Hii ni baada ya makabiliano makali kuzuka kati ya wanajeshi wa Somalia (Somali National Army-SNA) na wenzao wa Ukanda wa Jubaland.

Tukio hilo liliishia kutwaliwa kwa kambi ya kijeshi ya Ras Kamboni iliyoko Somalia karibu na mpaka wa Kenya.

Shambulizi hilo lilitokea Desemba 11, 2024.

Ni kutokana na makabiliano hayo makali ambapo wanajeshi walioshindwa nguvu Somalia walitoroka na kujificha kijijini Ishakani, nchini Kenya.

Wanajeshi hao walijisalimisha kwa wakazi, ambapo walisaidiwa kufika kwenye kambi za walinda usalama za Kenya, Ishakani.

Barkale Madi, mmoja wa wazee wa kijiji cha Ishakani, alikiri kupokea wanajeshi hao wengi wa Somalia waliofika kwa makundi usiku.

“Ilikuwa majira ya saa mbili jioni tuliposhtuka kuona wanajeshi wenye bunduki wakiwasili kijijini kwetu Ishakani kwa makundi. Tulishtuka. Baada ya kuwasikiliza tulitambua hao walikuwa watu waliohitaji msaada wetu. Nikawachukua hadi kambi ya walinda usalama wa Kenya. Walipojieleza na kuhakikiwa, walipokonywa bunduki na kisha kuruhusiwa kukaa shuleni Ishakani,” akasema Bw Madi.

Bw Madi pamoja na wenzake anasema waliendelea kuwapokea na kuwasaidia wanajeshi hao wa Somalia hadi saa nane usiku.

Alisema uwepo wa vyoo vichache ni miongoni mwa changamoto zilizowakabili wanajeshi hao wa Somalia kwani walikuwa wengi.

“Vyoo havikuwa vinatosha kwa siku hizo tano ambazo wanajeshi wa Somalia waliishi hapa. Na ndiyo sababu utapata vyoo vichache vilivyoko viliharibiwa, huku wanajeshi wengine wakiishia kwenda haja msituni. Tunahitaji ukarabati wa haraka na usafishaji wa mazingira yetu hapa kwani yalichafuliwa sana,” akasema Madi.

Fatma Ahmed, mkazi wa Ishakani, aliiomba serikali na wahisani kufika kijijini humo ili kukadiria hali ilivyo, akisisitiza haja ya miundomsingi kurekebishwa iliyoharibiwa.

“Maafisa hao walikuwa wengi, hivyo wengine walilazimika kuenda msituni kujisaidia. Tunahofia mlipuko wa kipindupindu. Tunahitaji usaidizi; Tutengenezewe vyoo vilivyochafuliwa na mazingira yetu yasafishwe,” akasema Bi Ahmed.

Wakati huohuo, Shirika la Msalaba Mwekundu tayari limewasilisha misaada ya chakula na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi kwa baadhi ya familia za Somalia zilizotorokea Kiunga, nchini Kenya kufuatia mzozo na makabiliano ya wanajeshi wa Somalia.

Mshirikishi Mkuu wa Msalaba Mwekundu, tawi la Lamu, Bw Abdulhakim Mahmoud alisema kuna jumla ya familia 343 za Somalia zilizosaka makao ya muda mjini Kiunga, ambapo tayari 108 zimepokezwa misaada.

“Tumewasilisha vyakula na mahitaji mengine kwa familia husika. Usaidizi bado unahitajika, hasa matibabu na chakula,” akasema Bw Mahmoud.

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*