Wakulima wa ngano Laikipia walalamikia bei ya chini sokoni – Taifa Leo


WAKULIMA wa ngano Kaunti ya Laikipia wanatoa wito kwa serikali kujenga maghala ya kuhifadhi nafaka katika vituo vya kukusanya ngano eneo hilo.

Wakulima hawa wanaamini mikakati hii itawaepusha na hasara ambazo hushuhudiwa katika msimu wa mavuno.

Vile vile, uhaba wa vituo vya ukusanyaji katika kaunti hiyo ni changamoto kwao kila wanapokadiria bei ya kuuza mazao yao.

Iwapo watahitaji kujitafutia sehemu ya kuhifadhi mazao yao, wakulima hawa hulazimika kusafiri hadi Nakuru kuliko Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB).

“Tuna zaidi ya magunia 30,000 ya ngano katika stoo zetu. Tunahitaji bei nzuri sokoni na mahali pa kuhifadhi. Ikiwa tungekuwa na kituo cha kujumlisha na maghala makubwa, tungesubiri bei ziwe nzuri. Tunategemea tu hifadhi ya Nakuru ambayo hujaa,’’ alilalamika Margaret Ndung’u, mkulima wa ngano.

Shamba la ngano likiwa karibu kuvunwa. Picha|Labaan Shabaan

Wakulima hao walikuwa wakizungumza mjini Nanyuki wakati wa mkutano wa Chama cha Wakulima wa Nafaka (CGA) mnamo Ijumaa.

Kulingana na Bi Ndung’u, bei ya sasa ya soko si nzuri kwa wakulima sababu wanabiashara wanaagiza kutoka nje ya nchi kwa ushuru wa chini.

Mkulima mwingine wa ngano Bw Kamweru Kinyua, alikariri kuwa wakulima wana ngano ambayo walilemewa kuuza na sasa wanakabiliwa na hasara.

Wakati huo huo, walibainisha kuwa serikali ilianzisha Mpango wa Ununuzi wa Ndani ambapo wasagaji wa ngano wa humu nchini wanaruhusiwa kuagiza ngano kutoka nje kwa ushuru wa chini wa asilimia 10.

Hii ni kinyume na ushuru wa asilimia 35 kulingana na Ushuru wa Pamoja wa kuagiza mazao kutoka nje kwa mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mkulima wa ngano John Sitienei. Picha|Labaan Shabaan

Katika msimu wa 2024 hadi 2025, bei ya chini iliyowekwa ya ngano inayozalishwa nchini ni Sh5,300 kwa gredi ya kwanza, na Sh5200 kwa gredi ya pili kwa gunia la kilo 90.

Hata hivyo, walilalamika kuwa wasagaji na madalali hununua ngano zao kwa Sh3300 tofauti na bei iliyotolewa na serikali.

Kulingana na ripoti kutoka Mamlaka ya Kilimo na Chakula nchini (AFA), ngano ni nafaka ya pili inayoliwa sana nchini baada ya mahindi.

Kenya huzalisha chini ya tani 500,000 za ngano huku nchi ikitumia tani milioni 1.7 za ngano kila mwaka.

Mkulima wa ngano John Sitienei aonyesha shuke la ngano lililo karibu kukomaa tayari kwa mavuno. Picha|Labaan Shabaan

Imetafsiriwa na Labaan Shabaan

Ends…



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*