Walimu, polisi walia bima ya matibabu kukatizwa – Taifa Leo


WALIMU, polisi na askari wa magereza wamelilia kukatiziwa huduma za kimatibabu kwenye hospitali mbalimbali kutokana na deni la Sh11.6 bilioni ambazo kampuni za bima zinadai serikali.

Kutokana na hali hii ya kusikitisha, baadhi ya walimu kutoka eneo la Bonde la Ufa na Nyanza wamepanga kuandaa mgomo leo.

Haya yanafanyika huku mazungumzo yakiendelea kuhakikisha kuwa huduma za kimatibabu kwa watumishi hao wa umma zinarejelewa kama kawaida.

Maafisa wa Chama cha Walimu Nchini (KNUT) na kile cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai (KUPPET), wamelalamikia wanachama wao kukosa matibabu kutokana na deni la serikali.

Haya yanajiri wakati ambapo Wakenya nao wamekuwa wakilalamikia kukosa huduma kutokana na kuanzishwa kwa Bima ya Afya ya Jamii (SHA).

Meneja wa Kampuni ya Minet ambayo husimamia bima ya walimu, Bw Edwin Kegode, alisema hospitali sita zimewaandikia kuwa zitaacha kuhudumia walimu lakini mazungumzo yanaendelea kupata muafaka.

“Tunaendelea kuzungumza na usimamizi wa hospitali hizo kuhakikisha huduma zinarejelewa huku tukifuatilia deni hilo na serikali,” akasema Bw Kegode.

“Tumekuwa na uhusiano mzuri na hospitali kwa miaka kadhaa na nina hakika kuwa suala hili ambalo limekuwa likijitokeza, litapata suluhu,” akaongeza Bw Kegode.

Minet iliingia kwenye mkataba wa kuwapa walimu huduma za bima kutoka Disemba 31, 2022 hadi Novemba 31, 2025.

Hazina Kuu ya Kifedha kukosa kuzilipa kampuni za bima kwa zaidi ya miezi saba, imefanya walimu na wakufunzi zaidi ya 452,635 wakose huduma za matibabu.

Kwa mujibu Shirika la Kitaifa la Takwimu Nchini (KNBS), Kenya ina polisi 109, 857 ambao wana bima ya matibabu.

Kampuni ya MAKL ndiyo inasimamia bima ya Sh8.67 bilioni kwa polisi na maafisa wa magereza.

MAKL hata hivyo imesambaza jukumu la kutoa huduma hizo za bima ya kimatibabu kwa kampuni za APA, CIC, Old Mutual na Britam.

Pia Minet imekuwa ikitumia kampuni za bima za Old Mutual, Britam, Pioneer, Bliss na Star Discovery kutoa huduma za bima kwa walimu.

Hata hivyo, idadi ya hospitali ambazo zimekuwa zikikataa kutoa huduma za kimatibabu kwa walimu zimeongezeka sana nchini.

Baadhi ya hospitali ambazo zimekataa kuwapa walimu huduma za kimatibabu hadi zilipwe hela zao ni AGC Tenwek na Chelymo zinazopatikana Kusini mwa Bonde la Ufa.

Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii (KTRH) na ile ya Raele Kaunti ya Uasin Gishu, pia zimekataa kuwahudumia walimu wakidai hela zao.

Kaskazini mwa Bonde la Ufa, maafisa wa Kuppet na Knut waliahidi kuwashinikiza walimu wagome wakisema kusitishwa kwa huduma kumewaathiri wanaougua magonjwa sugu kama kisukari na kansa.

“Inasikitisha kuwa tunakatwa pesa lakini haziwasilishwi ndiposa tumejipata kwenye hali hii,” akasema Bw Sammy Bor, mwanachama wa Baraza la Kitaifa la KNUT.

Bw Bor ambaye ni katibu wa Knut tawi la Chepkoilel aliwaongoza maafisa wa Knut na Kuppet katika kuvamia afisi za Minet Kaskazini mwa Bonde la Ufa kulalamikia kuondolewa kwa huduma katika hospitali za eneo hilo.

Kusini mwa Bonde la Ufa Katibu wa Kuppet tawi la Bomet, Bw Paul Kimeto na mwenzake wa Knut, Bw Desmond Lagat, waliandaa mkutano na maafisa wa MAKL na usimamizi wa hospitali ya Tenwek ili kupata maafikiano.

Wabunge Richard Yegon (Bomet Mashariki), Paul Chebor (Rongai), Victor Koech (Chepalungu), Richard Kilel (Bomet ya Kati) na Joseph Cherorot (Kipkelion Mashariki) Jumatatu walitoa wito kwa Hazina ya Kifedha itoe hela kwa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) pamoja na Huduma ya Kitaifa kwa Polisi (NPS) ili zilipe kampuni za bima.

“Hili ni suala ambalo linastahili kushughulikiwa kidharura ili walimu na polisi wasikose huduma za kimatibabu,” akasema Bw Yegon.

“Baadhi ya walimu wamelazimika kuitisha msaada kwa sababu hawawezi kumudu gharama ya matibabu,” akasema Bw Kilel.

Katibu Mkuu wa KNUT Collins Oyuu jana alisema kuwa wanaendelea kuzungumza na usimamizi wa hospitali ya AGC Tenwek kupata suluhu.

“Tunataka walimu watibiwe huku TSC ikishughulikia suala hilo,” akasema BW Oyuu.

Mwenyekiti wa KUPPET Omboko Milemba ambaye pia ni mbunge wa Emuhaya, naye alisema jambo muhimu ni Hazina Kuu kutoa pesa ili TSC nayo izilipe kampuni za bima.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*