WIKI moja tu baada ya shule kufunguliwa kwa muhula wa kwanza, walimu wakuu wameanza kuwatuma nyumbani wanafunzi wenye masalio ya karo.
Hii ni baada ya Serikali kukosa kutuma shuleni pesa za ufadhili wa shughuli za masomo, hali ambayo imewaacha walimu wakuu katika hali ngumu kuendesha shughuli za shule za umma.
Maafisa wa Chama cha Walimu wa Shule za Upili (Kessha), wakiongozwa na mwenyekiti wa kitaifa Willy Kuria walisema wanachama wao hawana jingine ila kuwatuma nyumbani wanafunzi.
Walimu wakuu walianza kufanya hivyo Ijumaa wiki jana wakisema hawana fedha za kuendeshea shughuli za masomo.
“Hatukupewa pesa za kutosha mwaka jana… kulikuwa na upungufu wa Sh7000 kwa kila mwanafunzi. Na kila mwaka kumekuwa na upungufu wa kiasi sawa na hicho. Kwa miaka mitano sasa serikali tunaidai serikali jumla ya Sh64 bilioni kuashiria kuwa shule zinakabiliwa na mzigo wa madeni,” akasema Bw Kuria.
Mwenyekiti huyo wa chama cha KESSHA alisema shule zilipofunga mwishoni mwa muhula wa tatu mwkaa jana, shule hizo hazikuwa zimewalipa Walimu walioajiriwa na Bodi za Shule, kutokana na ukosefu wa pesa.
Kwa mfano, Shule ya Upili ya Murang’a yenye jumla ya wanafunzi 1, 800 inazongwa na mzigo wa deni la Sh20 milioni za malipo ya umeme, maji na vifaa vingine vya masomo ilivyowasilishiwa na wafanyabiashara kwa mkopo.
“Madeni yetu yamekuwa yanaongezeka kwa sababu huwa tunalipa kidogo kidogo kutokana na changamoto za kifedha. Tumekuwa tukilipa baadhi ya madeni haya wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaporipoti. Lakini serikali inapokosa kutoa pesa za ufadhili wa masomo, huku tukiwa hatujui ni lini pesa hizo zitatolewa nasi hatuna uhakika wa kulipa malimbikizi ya mishahara,” Bw Kuria akasema.
Bw Kuria alisema, ambaye ni pia ndiye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Murang’a alisema hali ni ngumu kwa sababu Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza hawakusajiliwa kutokana na mpango unaoendelea kuwa kuondolea mbali mfumo wa elimu wa 8-4-4 kutoa nafasi kwa mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC).
Mwaka jana, 2024, hakukuwa na watahiniwa wa Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE), ishara kwamba hakuwa na uteuzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.
Kundi la mwisho la wanafunzi waliofanya KCPE wako katika kidato cha pili mwaka huu.
Mfumo wa Elimu wa 8-4-4 ulianzishwa 1985 ambapo wanafunzi walikuwa wakisoma kwa miaka minne katika shule za msingi, miaka minne katika shule za upili na miaka minne katika vyuo vikuu.
Kinyume na mfumo huo, mtaala wa CBC unatilia mkazo zaidi ujuzi, unafuata mfumo wa 2-6-3-3-3.
Kwa hivyo, mojawapo za sababu zinazochangia shule za upili kukumbwa na changamoto za kifedha ni ukosefu wa usajili wa wanafunzi wapya.
“Shule za mabweni hutegemea usajiliwa wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kupata pesa zaidi lakini mwaka huu hazijapata pesa hizo na ndio maana zinakumbwa na changamoto za kifedha,” Bw Kuria akaeleza.
Alisema shule za upili za kutwa ndizo zimeathiriwa zaidi kwa sababu zinategemea fedha kutoka kwa serikali kuendeshea shughuli zao ikizingatiwa kuwa hazitozi karo zozote.
Leave a Reply