ZAIDI ya wanafunzi 250 kutoka Kaunti ya Homa Bay sasa watajiunga na vyuo vya kiufundi baada ya kudhaminiwa na shirika moja lisilokuwa la kiserikali.
Kama njia ya kupambana na ukosefu wa kazi na kuwapa vijana ujuzi wa kiufundi, SHOFCO itatoa udhamini wa masomo kwa vijana hao.
Mwanzilishi wa Shofco Kennedy Odede alisema kuwa shirika hilo linamakinikia ufadhili wa kujiunga na vyuo vya kiufundi ili kuwapa vijana ujuzi wa kupambana na ukosefu wa kazi na kusaidia kwenye ustawi wa kiuchumi.
“Shofco japo inalenga kuondoa umaskini kupitia elimu na kupiga jeki jamii kiuchumi, pia inamakinikia kuwa kaunti hii inapiga hatua mbele kimaendeleo,” akasema Bw Odede.
Waziri wa Elimu (CEC) Homa Bay Martin Opere alitaja umuhimu wa ujuzi wa kiufundi na teknolojia katika kuhakikisha kuwa vijana wanajiajiri na kujikimu maishani.
“Baada ya kupata ujuzi huo wa kiufundi, vijana watakuwa na hiari ya kufanya kazi yoyote ile hasa kwenye viwanda mbalimbali. Ujuzi ndio suluhu kwa tatizo la ajira,” akasema Bw Opere.
Kando na ufadhili wa masomo, Shofco pia imetia mkataba na serikali hiyo ya kaunti kujenga kituo kikuu cha kuokoa waathiriwa wa dhuluma za kijinsia kwenye eneobunge la Mbita.
“Mpango huo tayari umeidhinishwa, stakabadhi hitajika kutiwa saini na kilichobakia sasa ni uzinduzi wa ujenzi huo kuanza Januari 2025,” akaongeza Bw Odede akiwa katika Kaunti ya Homa Bay.
Afisa huyo alisema Homa Bay ndiyo kitovu cha miradi ya Shofco Nyanza na tayari imechimba na kujenga mabwawa madogo 16 katika maeneobunge mbalimbali ya gatuzi hilo.
Mabwawa hayo husaidia kudhibiti mafuriko na pia maji hayo hutumika katika kilimo cha unyunyiziaji mashamba maji wakati wa ukame.
Imetafsiriwa na CECIL ODONGO
Leave a Reply