KUNDI la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi Jumatatu walifika katika makao makuu ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB), Nairobi kulalamikia kucheleweshwa kwa pesa hizo.
Wanafunzi hao waliokuwa na ghadhabu walivuruga usafiri wa magari katika barabara ya University Way karibu na afisi za bodi hiyo zilizoko katika jumba la Anniversary Towers.
Walitaka wahutubiwe na Afisa Mkuu Mtendaji wa HELB Charles Ringera, ambaye alikuwa akikutana na wadau afisini mwake.
Badala yake, Bw Ringera alimtuma Meneja wa Mikopo Joseph King’ori Ndegwa aliyewaambia wanafunzi hao kuwa kutolewa kwa pesa hizo kulicheleweshwa na kesi iliyoko katika Mahakama ya Rufaa.
Bodi ya HELB na Hazina ya Ufadhili wa Masomo ya Vyuo Vikuu (UF) ziliwasilisha kesi hiyo kupinga uamuzi wa mahakama kuu wa kwamba mfumo mpya wa ufadhili wa masomo katika taasisi hizo unakiuka katiba.
Bw Ndegwa alifichua, japo rufaa hiyo bado haijaamuliwa, HELB imekuwa ikitoa pesa za wanafunzi wa mwaka wa kwanza na pili kuanzia wiki jana, chini ya mfumo wa zamani.
“Sababu ya kucheleweshwa kwa pesa zenu ni kwamba kesi iliwasilishwa mahakamani na jaji akatoa uamuzi uliozima kabisa utekelezaji wa mfumo mpya wa ufadhili.
“Lakini ndani ya wiki mbili zilizopita tumetafuta njia nyingine ya kulipa pesa hizo,” Bw Ndegwa akasema.
Afisa huyo alieleza kuwa tangu Ijumaa wiki jana hadi jana asubuhi, bodi hiyo imetoa jumla ya Sh3 bilioni kugharimia matumizi ya wanafunzi.
“Tuliamua kuwapa wanafunzi pesa kwa kufuata mfumo wa zamani.”
Wakati huo huo, Chuo Kikuu cha TUK kilifungwa jana baada ya wahadhiri kugoma wakilalamikia kucheleweshwa kwa mishahara yao, miongoni mwa malalamishi mengine.
Kwenye taarifa iliyotolewa jana Afisa Msimamizi wa Masuala ya Masomo chuoni humo Dr Moses Wamalwa, wanafunzi wote wanaosomea kozi za diploma na shahada ya kwanza ya digrii walihitajika kuondoka saa nane na dakika 45.
Japo taarifa hiyo haikuashiria moja kwa moja kuwa chuo kikuu cha TUK kimefungwa, masharti kwamba wanafunzi hao waondoke yaliashiria kuwa hawaruhusiwi humo.
“Vile vile, wanafunzi wanaoishi katika mabweni ya chuo wanapaswa kuondoka ikifikapo saa kumi na moja jioni, Jumatatu, Februari 3, 2025,” taarifa hiyo ikaongeza.
Leave a Reply