ZAIDI ya wavulana 200 kutoka Shule ya Upili ya Wavulana ya AIC Cheplaskei walihatarisha maisha yao baada ya kutembea mwendo wa kilomita 20 hadi Makao Makuu ya Kaunti ya Uasin Gishu jijini Eldoret kupinga mpango wa kumhamisha mwalimu wao mkuu waliyemtaja kama mzazi stadi na msimamizi bora.
Wanafunzi hao waliojawa na ghadhabu walitembea kwa zaidi ya kilomita 20 kutoka Cheplaskei, kaunti ndogo ya Kesses hadi jijini Eldoret walishutumu baadhi ya wanachama wa bodi ya usimamizi kwa kuendeshwa na ukabila kupanga njama ya kuhamisha mwalimu wao mkuu kwa madai ya kuwa anatoka katika kabila jingine.
“Lengo letu ni kufaulu katika elimu hatujali mkuu wetu anatoka katika kabila gani, baadhi ya wafadhili wa shule yetu wameungana kupanga njama za uhamisho wa mkuu wetu mpya kwa manufaa ya baadhi ya wasimamizi wa shule yetu, iwapo watashawishi uhamisho wa mwalimu mkuu hatutakubali kukaa darasani,” alisema mmoja wa wanafunzi hao alipokuwa akihutubia Mkurugenzi wa Elimu Kaunti ya Uasin Gishu John Thiringi.
Kwa pamoja walitaka naibu mwalimu mkuu pamona mhasibu wa shule wahamishwe badala ya mwalimu mkuu.
Walidai kuwa wanaotaka mwalimu mkuu kuhamishwa hawapendi sera yake ya kutaka walimu kukamilisha silabasi kwa wakati hasa kwa watahiniwa wa Kidato cha Nne.
Wanafunzi hao ambao hawakuwahi kuhudhuria masomo tangu Jumatatu walifanya maandamano mafupi katika shule hiyo na kusababisha uharibifu wa mali.
Kwa pamoja walisema wanaridhishwa zaidi na Mwalimu Mkuu wao wa sasa, Bw Nathan Oguye ambaye amechukua nafasi ya mwalimu mkuu mstaafu George Oloo.
Bw Thiringi aliwaomba kurudi shuleni huku akiahidi kushughulikia matakwa yao.
Wanafunzi hao walirejeshwa shuleni kwa mabasi sita kutoka shule mbalimbali katika kaunti ya Uasin Gishu.
Leave a Reply