WATU wanaosababisha, kununua au kuhimiza watoto au watu wazima walio na ulemavu katika shughuli ya ombaomba watapigwa faini ya Sh2 milioni au kifungo cha miaka miwili jela baada ya Bunge kupitisha mswada mpya kuwa sheria.
Bunge la Kitaifa lilipitisha Mswada kuhusu Walemavu, Mswada wa Seneti Nambari 7 ya 2023, unaokusudiwa kuainisha sheria za Kenya na Kifungu 54 cha Katiba, kuimarisha haki na nafasi za walemavu.
Katika kikao maalum Alhamisi iliyopita (Januari 16, 2025), wabunge waliidhinisha marekebisho yaliyowasilishwa na Kamati kuhusu Ulinzi wa Jamii kuimarisha adhabu inayotolewa kwa wanaowatumia vibaya walemavu.
“Mtu anayesababisha, kununua, kuhimiza au kutuma mtoto au mtu mzima mwenye ulemavu kujihusisha na omba omba au kupokea misaada atapatikana na hatia baada ya kushtakiwa na kutozwa faini isiyozidi milioni mbili au kufungwa jela au yote mawili,” kinaeleza kipengee kipya cha mswada huo, ambao sasa unasubiri saini ya Rais William Ruto kuwa sheria.
Mswada huo unaimarisha adhabu kwa kuwatoza faini ya hadi Sh1 milioni, watu ambao kimaksudi au kwa kujua, wanafanya au kuruhusu walemavu kudhalilishwa kupitia maneno, matamshi, maandishi au ishara.
Awali, mswada huo ulikuwa umependekeza faini ya Sh200, 000 au kifungo cha jela kwa muda usiozidi mwaka mmoja kwa mtu anayefanya au kuruhusu kimaksudi au kwa kujua, kudunishwa kwa walemavu.
“Kwamba kipengee 66 cha Mswada kirekebishwe kwa kufuta maneno “Sh200, 000” na badala yake kuweka maneno “Sh1 milioni,” yanaelzea marekebisho ya Mswada huo.
Mswada huo unawazaba faini ya Sh2 milioni au kifungo cha mwaka mmoja gerezani wahudumu wa afya wanaowatelekeza walemavu.
Inawakataza wataalamu wa afya kuwabagua walemavu katika kuzingatia kanuni za kitaaluma kuhusu idhini na faragha wanapotoa huduma za afya na huduma nyinginezo kwa walemavu.
“Mtu yeyote anayefanya au kuelekeza shughuli yoyote ya matibabu kwa mlemavu, inayosababisha au iliyo na uwezo wa kusababisha utasa anatenda hatia na atatozwa faini ya Sh3 milioni au kufungwa jela kwa muda usiozidi mwaka mmoja au zote mbili,” unasema Mswada.
Imetafsiriwa na Mary Wangari
Leave a Reply