Wanasiasa wawaruhusu Wakenya wawatusi ili hasira ziwatoke – Taifa Leo


NAAMBIWA mtu amekariri kwamba anakichukia chama tawala anavyoichukia karatasi ya sashi aliyokwisha kuitumia!

Dah! Si hayo ni maelezo ya karibu sana kuhusu shughuli inayoendelea faraghani, ndani ya chumba cha mtu yeyote mstaarabu?

Mbona mtu atumie mfano wa aina hiyo? Kwani mtu huangalia sashi akishaitumia? Au labda anachukulia kwamba ni mbaya mno, haiangaliki?

Nadhani mtu akiamua kutoa mfano kama huo huwa amefika mwisho, hivyo anapaswa kusaidiwa si kukashifiwa. Msaada wake ni rahisi; mwambie apunguze hasira, atwambie iwapo kwa hakika amekosa mifano bora.

Akisema amekosa, basi jua anakaribia kulipuka, umpe maji ya baridi, umpumzishe kivulini, umwambie avute pumzi ndani kisha azitoe nje, asipopata nafuu umwitie gari la wagonjwa akasaidiwe spitalini.

Ngoja kidogo… labda nakupa kazi ngumu. Magari ya wagonjwa ni nadra sana vijijini. Labda toroli za Kasongo zingaliko kwa kuwa hafanyi kampeni ya ‘mama mboga’ tena, hivyo twaa moja umsukume hadi katika zahanati ya karibu.

Serikali na wanasiasa kwa jumla wanafaa kuwaruhusu Wakenya wawatusi ili hasira ziwatoke. Badala ya watu kuvimba na kulipuka ghafla kama mabomu, ni heri waruhusiwe kutoa pumzi polepole kwa njia ya matusi.

Anayetukana leo akaachwa, aghalabu kesho hana tusi jingine. Hata hivyo, ukimzuia kutukana, na labda ana tusi moja pekee analodhani kuwa kali mno, mtasumbuana kwa muda.

Watu wanaotukana serikali yao huhisi vizuri wakienda nyumbani salama bila kukamatwa na kutoweshwa, lakini wanaobanwa na kukandamizwa kwa kila njia huanza kufikiria kuhusu wanavyoweza kuing’oa serikali mamlakani.

Kutema matusi, japo machafu kabisa, ni sehemu ya uhuru wa kujieleza katika ulimwengu wa wanyonge. Mnyonge asiye na uwezo wa kukushtaki wala kukupiga akikutusi, nawe umpuuze, huhisi amekukomesha.

Jaribu kuwa mtu mzima, utukanwe na kupuuza, ujiambie tusi halinati nguoni kama sumaku. Utakuwa umemsaidia mnyonge kupata nafuu.

Unajua vyema ukimtia mkononi unaweza kumsaga kama unga wa mahindi, lakini hutaki kufanya hivyo kwa sababu utafungwa jela, utafunwe na chawa, ule ugali na maharagwe yasiyoiva vyema, uvimbiwe.

Lakini ukimwacha ende zake, kuna uwezekano mkubwa kwamba kesho mkikutana atakuwa ameishiwa na matusi, tena atainamia chini kwa haya, hatataka nyuso zenu zikutane.

Utakuwa umemshinda. Hata unaweza kumwambia ajaribu tusi jingine, lile la jana halikukuachia kovu. Akijasiria kujaribu jingine, lichukulie vile-vile tu.

Siku ya tatu akikuona njiani ukija atakata kona na kuchana mbuga ili asikutane na mtu ‘mjinga’ kama wewe. Nina hakika kufikia sasa unajua mjinga ni nani kati yenu.

Katika nchi ambapo masaibu yanasababisha msongo wa mawazo, matusi dhidi ya serikali na wanasiasa yanapaswa kuhalalishwa kama mojawapo ya njia za watu kupumulia.

Wala asikwambie mtu eti utundu utaongezeka! Ni sawa na sigara ilivyohalalishwa. Je, sote ni wavutaji? Atakayetukana sana atakuwa anatukumbusha kwamba mama yake hakumfunza vyema.

Dunia ina fursa ya kumfunza nidhamu kwa kumpa jukwaa, acheze aache jina, mwishowe atambue kuwa matusi ni muhimu kwake pekee.

[email protected]



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*