WAPELELEZI kutoka Kitengo cha Mauaji katika Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu DCI wameanzisha uchunguzi kuhusu mauaji ya mwanaharakati wa Molo ambaye alikuwa mkosoaji wa serikali.
Haya yanajiri huku ikiibuka kuwa wanasiasa wawili wa eneo la Molo na mashahidi kadhaa ni miongoni mwa watu ambao wapelelezi wanapanga kuhoji katika juhudi zao za kubaini sababu za mauaji ya Richard Otieno, almaarufu ‘Molo president’.
“Tutahoji mashahidi kadhaa na wanasiasa wawili, tukijaribu kuelewa sababu ya mauaji haya ya kikatili,” alifichua mmoja wa maafisa wanaohusika na uchunguzi.
Bw Otieno, ambaye pia alikuwa kiongozi wa vijana alikuwa mkosoaji wa serikali na Mbunge wa Molo Bw Kuria Kimani, aliuawa Jumamosi usiku kwa kukatwakatwa, mita chache kutoka Kituo cha Polisi cha Elburgon.
Siku mbili kabla ya mauaji hayo, Bw Otieno alilalamikia kupokea vitisho na kufuatwa na watu watatu wasiojulikana.
Taifa Leo imefahamu kuwa maafisa kutoka Kitengo cha Mauaji cha DCI wameanza kutegua kitendawili cha kifo hicho.
Jumanne, timu ya maafisa kutoka kitengo hicho, ikiongozwa na Bw Martin Nyuguto, ambaye ni mkurugenzi wa kitengo cha mauaji ilitembelea eneo la tukio ambapo marehemu aliualiwa.
Wakili wa Familia ya marehemu Bi Roselinda Wamaitha alisema wapelelezi hao walikutana na familia, kuihakikishia kuwa uchunguzi wa kina utafanyika na wahusika watakamatwa.
“DCI inachunguza mauaji haya ya kinyama. Wanakusanya taarifa zitakazosaidia kutegua mauaji haya ya kutatanisha na kuwatia mbaroni wauaji,” alisema Bi Wamaitha.
Kamanda wa polisi wa Molo Timon Odingo, alisema wapelelezi wana vidokezo vitakavyosaidia kuwatia mbaroni wahusika.
“Naomba umma utulie uchunguzi wa mauaji haya ukiendelea. Umma usijihusishe na uvumi kuhusu mauaji haya kwa kuwa wapelelezi watawatia mbaroni wauaji,” alisema Bw Odingo.
Mmoja wa wapelezi alifichua kuwa wanachunguza vitisho alivyopokea marehemu, na kuwatafuta watu watatu wasiojulikana waliodaiwa kumfuata Alhamisi iliyopita kabla ya kuuawa Jumamosi.
Sehemu muhimu ya uchunguzi, pia itakuwa upasuaji wa maiti unaotarajiwa kufanywa wiki hii na mtaalamu wa upasuaji wa serikali, Bw Johansen Oduor.
Taifa Leo imebaini kuwa zaidi ya watu watano tayari wameandika taarifa zitakazosaidia wapelelezi katika uchunguzi wao.
Jumapili, mamia ya wakazi walifika katika mochari ya hospitali ya kaunti ndogo ya Elburgon na kuchukua mwili wa marehemu kwa muda wa saa tano hadi nje ya kituo cha polisi cha Elburgon.
Hata hivyo, Bw Odingo alisema mwili huo ulihamishwa hadi Mochari moja kaunti ya Kericho.
Leave a Reply