
WANAWAKE waliopigania uhuru wa Kenya wakati wa Mau Mau sasa wanahisi kusalitiwa na taifa lile walilolikomboa.
Jane Njeri Mwangi, mwenye umri wa miaka 95, anasimulia jinsi serikali ilivyoharibu sio tu nyumba yake ya miaka 61 katika makazi ya Mathare, Nairobi, lakini pia kumfanya akose imani katika nchi ambayo alipigania kuikomboa.
Kwa sasa, anaishi katika kibanda kimoja karibu na uwanja wa umma Mlango Kubwa, Mathare.
Tangu siku hiyo, mama huyo anategemea marafiki ili kupata huku yeye pamoja na wajukuu wake wakihama kutoka kwa nyumba moja hadi nyingine.
“Nilishtuka sana, nilipotoka nje ya nyumba. Nilihisi kana kwamba tingatinga lililokuwa likibomoa makazi yangetufikia,” Bi Njeri anasema.
Alipoulizwa kuhusu hofu yake siku hiyo, alijibu, “Bila shaka. Kama binadamu, lazima uogope, kwa sababu riziki yako, nyumba yako – kila kitu kimechukuliwa. Ukatiliki mtupu.”
Anasema kuwa nyumba yake ilikuwa umbali wa mita 30. Hii ni baada ya serikali kutoa agizo nyumba zilizojengwa karibu na mto zibomolewe.
Hata wakati wa mafuriko makubwa ambayo yaligharimu maisha ya zaidi ya watu 10 huko Mathare na 200 kote nchini Kenya, makazi yake ya kawaida yalibaki bila kuathiriwa na mafuriko.
Mnamo Aprili 30, 2024, agizo maalum la Baraza la Mawaziri liliwapa wakazi wanaoishi kwenye maeneo yaliyo karibu na mto Mathare – saa 48 tu kuhama.
Wizara ya Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa kisha ikapunguza muda huu ambao tayari haukuwezekana, na kuamuru mtu yeyote ndani ya ukanda wa mto wa mita 30 kuondoka ndani ya saa 24.
Bi Njeri hakuwahi kujua kuwa angefikiwa na jambo kama hilo tangu aifanye eneo la Mathare kuwa makao yake mwaka wa 1963.
Kwa Njeri, ambaye alianza kuishi Mathare kama mpiganaji wa Mau Mau, usaliti huu wa hivi punde umemshangaza sana.
“Tulipigania uhuru wa nchi na ardhi yetu. Lakini sasa mambo yamekuwa tofauti. Ahadi tulizopewa sasa zimebaki kuwa stori.”
Bi Njeri anawawakilisha takriban wanawake 50 wa Mathare walioachwa bila makao baada ya agizo la serikali ya kubomoa nyumba au makazi yaliyo karibu na mito.
Wanawake thelathini kati ya hawa, kama Bi Njeri, walipigania uhuru wa nchi.
Leo, wanasimama kwa umoja kudai fidia na kuhamishwa kwao kutoka makazi yao. Walishirikiana na Kituo cha Haki ya Kijamii cha Mathare, shirika la kijamii la mashinani, kuwasilisha ombi kwa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu nchini na Wizara ya Ardhi na Makazi.
Leave a Reply