WAOMBOLEZAJI katika mazishi ya mwanawe aliyekuwa seneta wa kaunti ya Embu Lenny Kivuti, marehemu Eric Mutugi, jana walikataa ujumbe wa rambirambi kutoka kwa Rais William Ruto aliomtuma waziri wa Utumishi wa Umma, Bw Justin Muturi kuwasilisha.
Waziri Muturi alikuwa amesimama kusoma ujumbe huo wakati waombolezaji waliposimama kumkataza.Waombolezaji walisema hawakutaka ujumbe huo na kumwambia Bw Muturi aketi chini.
Bw Muturi alilazimika kukabidhi rambirambi za rais kwa familia ya Kivuti.Alipokuwa akikabidhi familia ujumbe, waombolezaji walishangilia na kupiga makofi kwa sauti kubwa huku makasisi wakimtazama kwa mshangao.Askofu Mkuu wa Kanisa Kianglikana Jackson Ole Sapit alitaka vitendo vya utekaji nyara vikomeshwe nchini.
Akiongoza ibada ya mazishi, Ole Sapit alisisitiza ili amani iwepo, Wakenya hawafai kutoweka kwa njia ya kutatanisha.Bw Mutugi, mtoto wa kwanza wa Bw Kivuti alifariki baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua na wabunge wa eneo hilo Eric Muchangi ( Runyenjes), Gitonga Mukunji ( Manyatta) Nebart Muriuki ( Mbeere Kusini) na Geoffrey Ruku walihudhuria.
Kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa alionya kuwa Wakenya watafanya maandamano kote nchini mnamo Machi 8 ikiwa vijana waliotekwa nyara hawatakuwa wameachiliwa wakiwa hai.’Ikiwa vijana waliotekwa nyara hawatapatikana wakiwa hai serikali itawajibishwa,’ alisema Wamalwa.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply