
SHOKA la Rais William Ruto limeanza kuwaangukia wandani wa aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua katika Seneti siku mbili baada ya bunge hilo kurejelea vikao vyake baada ya likizo ndefu ya Krimasi na Mwaka Mpya.
Maseneta Joe Nyutu (Murang’a), Karungo wa Thang’wa (Kiambu), John Methu (Nyandarua), James Kamau Murango (Kirinyaga) na Seneta wa Kajiado Lenku Seki wametimuliwa kama wenyeviti wa kamati muhimu za bunge hilo.
Kulingana na orodha ya maseneta walioteuliwa kuwa wanachama wa kamati mbali mbali iliyowasilishwa na kiranja wa walio wengi Boni Khalwale Alhamisi, watano wameondolewa katika kamati walizokuwa wakiongoza mwaka jana.
Bw Nyutu ametimuliwa kutoka Kamati ya Elimu, Bw Thang’wah ameondolewa kutoka Kamati ya Uchukuzi, Bw Methu ametimuliwa kutoka kamati ya Ardhi, Bw Murango hayuko tena katika Kamati ya Kilimo huku Bw Seki akiondolewa kutoka Kamati ya Biashara.
Kamati hizo ni muhimu kwani ndizo huhakikisha utendakazi wa wizara husika za Serikali Kuu.
Masene hao watano hao ni miongoni mwa maseneta waliopinga hoja ya kumtimua Bw Gachagua katika Seneti Oktoba mwaka jana.
Tangu wakati huo, wanasiasa hao waliochaguliwa kwa tiketi ya chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) wamekuwa wakishirikiana na Bw Gachagua kuikosoa serikali ya Rais Ruto.
Seneta wa Busia Okiya Omtatah Okoiti ambaye ametangaza azma ya kumpinga Rais Ruto kwenye kinyang’anyiro cha urais 2027 pia ametimuliwa kutoka Kamati ya Seneta kuhusu Uhasibu (CPAC).
Kamati hiyo ni yenye umuhimu mkubwa kwa sababu ndio huita magavana kufika mbele yake na kujibu maswali kuhusu matumizi ya fedha za umma katika kaunti zao, yanavyoibuliwa na Mhasibu Mkuu wa Serikali.
Katika Bunge la Kitaifa, wandani wa Bw Gachagua pia wanatarajiwa kuondolewa kutoka Kamati yenye hadhi.
Miongoni mwa wanaotarajiwa kutimuliwa ni Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya ambaye amekuwa akihudumu kama mwenyekiti wa Kamati kuhusu Biashara.
Mwingine ni Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba ambaye amekuwa akihudumu kama mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Utekelezaji wa Katiba (CIOC).
Duru zinasema kuwa Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro pia huenda akapoteza nafasi yake kama mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti.
Hii ni kwa sababu yeye ni miongoni mwa wabunge waliokwepo kufika bungeni mnamo Oktoba 8, 2024 kupiga kura ya kuunga mkono hoja ya kumtimua Gachagua, kulingana na agizo la Rais Ruto.
Leave a Reply