RAIA wa Congo ni miongoni mwa watu sita walioshtakiwa Ijumaa kwa ulaghai wa zaidi ya Sh262 milioni katika kashfa za dhahabu.
Wafanyabiashara hao Eric Kalala Mukendi (raia wa Congo), Steve Okoth Odek na David N Bett walishtakiwa mbele ya Hakimu Mwandamizi Gilbert Shikwe kwa kushiriki katika biashara feki ya dhahabu.
Hakimu alifahamishwa na Kiongozi wa Mashtaka Bi Judy Koech kwamba washtakiwa walijifanya walikuwa na maelfu ya kilo za dhahabu za kuuzia kampuni za kibiashara.
Wengine walioshtakiwa kwa kula njama za kulaghai Kampuni ya Aaz ShineGold & Diamond LLC Sh12,900,000, ni Nazlin Karim Rahimbux, Hubrand Kanyango Ndong’o, Susan Wanjeri Kogi na Elvis Ouma Muga.
Wanne hawa walikabiliwa na shtaka la kula njama za kuilaghai Kampuni ya Aaz ShineGold & Diamond LLC wakidai walikuwa na uwezo wa kuiziuzia kilo 20 za dhahabu.
Washtakiwa walikana shtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000 pesa tasilimu baada ya wakili Danstan Omari kudai “wanne hao ni watu wasio na mapato ya juu.”
Naye Eric Kalala Mukendi alikabiliwa na shtaka la kuibia kampuni ya Tanner Caldwell Sh223,756,000 akidai angeuza kilo 2820 za dhahabu.
Mahakama ilielezwa mshtakiwa alijua hakuwa na uwezo wa kuuzia Tanner dhahabu hiyo.
Mukendi alidaiwa alifanya kosa hilo kati ya Machi 31 na Mei 30, 2024 jijini Nairobi.
Leave a Reply