WATU wawili wanauguza majeraha katika hospitali ya Wema Kawangware na hospitali ya Eagle Kangemi kutokana na mlipuko kutoka kwenye kituo cha kuuza petrol na gesi na kuteketeza nyumba 28 Kawangware 56, Dagoretti Kaskazini, usiku wa kuamkia Jumamosi, Januari 4, 2025.
Tukio hilo, liliacha familia nyingi bila makazi na wafanyabiashara wakihesabu hasara.
Kulingana na mmiliki wa nyumba hizo Bi Phyllis Waithera, walisikia sauti ya kutisha ambayo iliwalazimisha kutoka nje na kupata duka la petrol likiteketea.
“Mwanzoni tulisikia sauti kama ile ambayo unafungua mtungi wa gesi, Kisha ukafuata mlipuko,” alisema Bi Waithera.
Mlipuko huo ulisababisha hofu, wapangaji wakakimbia ili kuokoa maisha yao. Wengi wao walikimbilia maeneo ya Muslim na Kangemi kutafuta hifadhi na usalama.
“Wale tuliobaki hatukuweza kuokoa chochote. Majirani kwenye ploti zingine ambao walidhania mto huo ungewaathiri walijaribu kuokoa mali zao, lakini zikaibiwa,” aliongeza Waithera.
Miale ya moto huo iliongeza hofu zaidi, familia zikaachwa zimeduwazwa na kutengana. Wengine walipata majeraha mabaya.
Miongoni mwa waliojeruhiwa ni dadake Damaris Maurice, ambaye aliokolewa ndani ya nyumba hizo. Bi Damaris alisema dadake alipoteza fahamu huku akipata majeraha ya moto kwenye miguu.
“Dadangu hawezi zungumza kwa sasa pale hospitalini. Sasa hivi nipo kwenye harakati ya kutafuta wanawe wawili, ambao bado hawajulikani walipo,” alisema kwa huzuni Bi Damaris.
Kisa hicho kiliwaacha wafanyabiashara bila chochote. Bw Samson Kamau, ameripoti kupoteza Sh700,000 pesa taslimu ambazo alikuwa ameweka kwenye meza ili kuwalipa wasambazaji wake. Hasara hiyo imemwacha Kamau katika hali ngumu kifedha, bila bima ya biashara au pesa alizokuwa ameweka.
“Nilitoka kwenda kuoga, nikipanga kurudi baadaye kulipa madeni. Baada ya duka la petroli kushika moto, miale ilienea hadi dukani mwangu, na nikapoteza kila kitu,” alieleza kwa masikitiko.
Duka lake, ambalo lilikuwa chanzo kikuu cha maisha kwa familia yake, liliungua kabisa, na kumwacha bila rasilimali za kuanza upya.
“Pesa hizo zilikuwa zinalenga kulipa madeni ya wasambazaji wangu. Sasa, ninakabiliana na changamoto ya kujenga upya duka langu bali pia na deni kutoka kwa wale wanaonidai,” aliongeza.
Licha ya uharibifu huo mkubwa, wakazi walitoa pongezi kwa wazima moto ambao walifanikiwa kudhibiti moto huo na kuzuia uharibifu zaidi.
Mzee wa Nyumba Kumi Bw Patrick Mukoa, alisema magari matatu hayo yalifika dakika 30 baada ya moto kuanza.
“Gari la kwanza lilimaliza maji, lakini gari la pili na tatu yalifanikiwa kuzima moto. Ingawa wakazi walijaribu kutumia maji mwanzoni, hayakutosha,” alisema Bw Mukoa.
OCPD wa Dagoretti, Kavinda Kilonzo, alithibitisha kuwa uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo cha moto huo.
“Ripoti ya awali inaonyesha kuwa moto ulitokana na mlipuko kwenye duka ambalo linawauzia wahudumu wa pikipiki petrol na gesi kwa wakazi. Watu wawili walipata majeraha kufuatia tukio hilo,” alisema Bw Kilonzo.
Kwa sasa, serikali imeanza kuandikisha majina ya waathiriwa ili kuona jinsi ya kupokea msaada.
Leave a Reply