Wauguzi watii agizo la korti na kurejea kazini – Taifa Leo


WAUGUZI waliokuwa wamegoma katika Kaunti ya Mombasa wamerudi kazini kufuatia agizo la mahakama ya Ajira na Masuala ya Leba (ELRC).

Chama cha Kitaifa cha Wauguzi nchini (KNUN), kilimwambia Jaji Monica Mbaru, kuwa wanachama wake wamerudi kazini, msimamo ambao ulithibitishwa na Serikali ya Kaunti ya Mombasa kupitia wakili wake.

Serikali ya Kaunti ya Mombasa ilikuwa imeshtaki chama hicho cha wauguzi ikitaka wauguzi hao wazuiwe kufanya mgomo.

Kupitia kwa wakili Murtaza Tajbhai, Kaunti iliiambia mahakama kuwa kutakuwa na mkutano wa pande zote mbili Jumanne mchana na walikuwa na matumaini ya kuwa utasuluhisha masuala kuhusiana na mgomo huo.

Mkutano huo ulikuwa haujakamilika kufikia wakati wa kuchapisha taarifa hii.

Kupitia kwa wakili wao, chama cha wauguzi kiliiambia mahakama kuwa kiko tayari kusuluhisha mambo yanayohusu mgomo huo kupitia mazungumzo.

“Mahakama imeona na kukubali juhudi mwafaka baina ya pande zote mbili ya kuzungumza na kusuluhisha hili suala,” alisema Jaji Mbaru pande zote mbili zilipofika mbele yake Jumanne.

Ijumaa iliyopita, ELRC ilikuwa imeagiza wauguzi hao wanaogoma mjini Mombasa kurudi kazini ili kupatia mahakama nafasi ya kusikiza masuala yanayowakumba kwa kuyapa kipau mbele.

Jaji Mbaru pia aliagiza kuwa wauguzi hao warudi kazini bila masharti yoyote.

Pia aliagiza Serikali ya Kaunti ya Mombasa kuwajali wauguzi wote walio kazini ikizingatiwa kuwa wanatoa huduma muhimu sana kwa wanananchi.

“Mahakama itaipa kesi hii kipaumbele…na kwa sasa mazungumzo yanayoendelea vile KNUN wamesema yarudi,” alisema jaji huyo.

Kupitia kwa wakili Tajbhai, serikali ya kaunti pia inataka agizo la kudumu la kuzuia chama hicho cha wauguzi na wanachama wake kuendelea na notisi ya mgomo ya Disemba 16, ambao ulianza Januari 13.

Serikali ya Kaunti ya Mombasa inasema kuwa, imechukuwa hatua mwafaka za kuhakikisha maslahi ya wauguzi yamesimamiwa na kulindwa.

“Serikali ya kaunti imechukuwa hatua zote mwafaka kuweka mazingira mazuri kwa wanachama wa Knun na inaedelea kufanya hivyo,” serikali ya kaunti ilisema katika stakabadhi zake za kesi.

Serikali hiyo ya kaunti pia inasema kuwa mgomo wa wauguzi hao ni haramu, unazuiwa na haulindwi.

Kaunti hiyo pia inasema kuwa, kile wauguzi wanajaribu kutatua kupitia mgomo kinaweza kutimizwa kwa wakati lakini maisha ya maelfu ya wakazi wa Mombasa ambao ni wagonjwa mahututi na wanapata matibabu hawana muda na madhara yake hayawezi kurekebika.

Serikali hiyo ya kaunti pia imesema haikuwa na mkataba wowote wa makubaliano baina yake na KNUN na kwamba mgomo huo haulindwi kisheria. Jaji Mbaru ameagiza kesi hiyo kutajwa mnamo Januari 28.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*