![wamumbi.jpeg](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2025/02/wamumbi-678x381.jpeg)
ZAWADI ya Sh1 milioni kutoka kwa Rais William Ruto zilizowasilishwa na Mbunge wa Mathira Eric Wamumbi katika Kanisa moja mjini Karatina, Nyeri, Jumapili ilipokelewa kwa manung’uniko na waumini.
Badala yake, walimtaka mbunge huyo amheshimu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwani ndiyo mlezi wake kisiasa.
Hayo yalijiri huku nipe nikupe kuhusu siasa za Mlima Kenya zikishamiri kati ya wafuasi wa Bw Gachagua na Rais Ruto wakati wa ibada katika kanisa hilo.
Rais Ruto alitarajiwa kuhudhuria Sherehe ya Ukumbusho wa Kuanzishwa kwa Kanisa la Victor Chapel linaloongozwa na Askofu William Githinji ila akakosa kufika huku uvumi ukienea kuwa angezomewa.
Kanisa hilo liko katika eneo bunge la Mathira anakotoka naibu wake wa zamani aliyegeuka hasidi wake mkuu kisiasa.
Hata hivyo, katika hotuba yake, Bw Wamumbi alijaribu kuelezea sababu iliyochangia Rais kutofika katika sherehe hiyo akieleza alibanwa na shughuli rasmi nchini Tanzania.
“Nimeona watu fulani wakidai kuwa rais alikwepa sherehe hii kwa sababu inafanyika katika ngome ya mtu fulani. Ningependa kuwaambia kuwa Rais yuko huru kutembelea sehemu yoyote ya nchi. Rais Ruto alitaka kuwa hapa lakini alibanwa na shughuli ya dharura kuhusu vita nchini DRC. Lakini amenituma na zawadi yake ya Sh1 milioni,” Mbunge huyo alisema.
Lakini alipowasilisha bunda la noti kwa Askofu Githinji, waumini hawakushangilia kwa furaha ilivyotarajiwa. Ni wachache tu walichangamkia zawadi hiyo huku wengi wakisikika wakinung’unika, ishara ya kuikataa.
Baada ya Rais Ruto na Bw Gachagua kukosana, wabunge wandani wa Dkt Ruto wamekabiliwa na wakati mgumu kutembelea maeneo bunge yake wakihofia usalama kufuatia hofu ya kushambuliwa na wafuasi wa naibu huyo wa rais wa zamani.
Wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z Juni mwaka jana, waandamanaji wenye ghadhabu walivamia makazi ya Bw Wamumbi katika kijiji cha Kamunyaka kwa kupigia kura Mswada wa Fedha wa 2024.
Ushawishi wa Bw Gachagua ni ukubwa zaidi katika eneo bunge la Mathira ambako amehudumu kama mbunge kati ya 2017 na 2022 ambapo alipanda ngazi kuwa Naibu Rais.
Lakini Wamumbi haelewani kisiasa na Bw Gachagua na wawili hao wamekuwa wakilumbana kila mara.
Bw Gachagua anamshutumu mbunge huyo wa Mathira kwa kutumiwa na mahasidi wake wa kisiasa kumhujumu.
Katika hotuba yake kanisani, Bw Wamumbi alipuuzilia mbali tangazo linalosubiriwa kwa hamu ambalo Bw Gachagua anasubiriwa kutoa akisema wakazi wa Mlima Kenya hawatamfuata “kikasuku”.
“Nasikia kuwa kuna watu fulani wanaodai kuwa wanalenga kutoa mwelekeo kwa watu wa Mlima Kenya. Hebu niwaulize, ikiwa alishindwa kulinda kiti chake cha naibu rais alipotimuliwa, sasa nani atampa mwelekeo? Huu ni ulaghai wa kisiasa,” akasema.
Hata hivyo, wandani wa Bw Gachagua wakiongozwa na diwani wa wadi ya Kirimukuyu Anthony Ndagita walimkabiliwa Bw Wamumbi wakimtaka amheshimu Bw Gachagua ambaye ni mlezi wake kisiasa.
“Tunapoitaka serikali iwajibike kwa wananchi, tunaposema kuwa mambo hayaendi vizuri, tusichukuliwe kama watu wanaoshambulia serikali. Gachagua ni shujaa wa uwajibikaji na ninamtaka mbunge wetu kumheshimu naibu rais wa pili aliyemlea kisiasa,” Bw Ndagita.
IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA
Leave a Reply