WAZAZI sasa wanataka Mabunge ya Kitaifa na Seneti, yaingilie kati na kusuluhisha utata unaotokana na amri ya Mdhibiti wa Bajeti (CoB) ya kuzuia magavana kutoa ufadhili wa masomo maeneo yao.
Magavana wiki jana walizimwa kutoa basari kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na taasisi za elimu. Wamewasilisha suala hilo kwa Baraza la Bajeti na Uchumi (IBEC) wakitaka amri hiyo iondolewe.
Muungano wa Kitaifa wa Wazazi (NPA) unataka mabunge ya Seneti na Kitaifa, yabuni sheria zitakazoongoza kutolewa kwa basari. Mnamo Januari 14, Mdhibiti wa Bajeti Dkt Margaret Nyakang’o aliwazuia magavana kutoa basari, hatua ambayo imepingwa vikali na wakuu hao wa kaunti.
Hata hivyo, Mwenyikiti wa Kamati ya Kiufundi ya Idara za Serikali (IGRTC) Githinji Gitahi ametoa wito kuwe na mkutano utakaoshirikisha Baraza la Magavana (COG), COB na IBEC kusuluhisha utata huo.
IBEC inaongozwa na Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki kama mwenyekiti wake.“Wanastahili waje IBEC na waseme walichokubaliana. Kwa sasa tunahitaji msimamo kamili wa COB kuwa basari itatolewa kwa wanafunzi kwa sababu muhula unaendelea na hakuna muda mwingi wa kujadiliana kuhusu suala hili,” akasema Bw Githinji.
Mwenyekiti huyo pia alitoa wito kwa Wizara ya Elimu kuchukua jukumu na kusaidia katika upatikanaji wa suluhu kuhusu suala hilo.
“Hatuna rasilimali za kufanya kila jambo na tunaitaka Wizara ya Elimu iwe mstari wa mbele katika kupata suluhu kwa suala hili,” akaongeza Bw Githinji.
Magavana wamekuwa wakitenga mamilioni ya pesa kugharimia basari za elimu ya wanafunzi. Hata hivyo, COB inasema kuwa elimu ya chekechea ndiyo imegatuliwa na ufadhili wowote unastahili kuelekezwa kwa sekta hiyo.
Leave a Reply