‘Wazee’ waonyeshana ubabe mashindano ya kuogelea Kiambu – Taifa Leo


SHIRIKISHO la Mashindano ya Kuogelea la Kaunti ya Kiambu (KCAA) liliandaa mashindano ya kufana ya waogeleaji waliozidi umri wa miaka 25, almaarufu Masters, katika shule ya Potterhouse School mtaani Runda, Kiambu, Jumamosi.

Zaidi ya washiriki 172 kutoka klabu na shule walijitokeza kwa mashindano hayo ya siku moja akiwemo Esther Kariuki, 72, aliyekuwa na umri wa juu kuliko waogeleaji wote waliojitosa bwawani kuonyesha ujuzi wao.

Jacqueline Macharia, ambaye ni kocha wa timu ya Harpoons na alikuwa akiogelea katika kitengo cha washiriki kati ya miaka 30 na 34, alitawala mbio za mita 100 kwa dakika 1:47.05.

“Tunatatizika kupata washiriki wa mashindano ya Masters kwa sababu wengi wanabanwa na majukumu yanayofanya wakose kuja mazoezi. Pia, wanatatizika na mabadiliko ya hali ya anga. Hata hivyo, nafurahia kuona idadi nzuri imejitokeza leo kwa mashindano ya Kiambu,” akasema Macharia.

Esther Kariuki, 72, aonyesha ujuzi wake wakati wa mashindano hayo. PICHA | HISANI

Maina Muriuki, 59, kutoka United Swim Club aliongeza kuwa mashindano hayo ni fursa nzuri ya watu wa rika lake kujiweka vyema kimwili na kuimarisha ushindani wao katika kuogelea kwa kurekebisha sehemu wamelegea. Muriuki alitawala 100m kwa 1:51.63.

Kariuki alisema amekuwa akichukulia uogeleaji kama tiba na kujiweka imara kimwili. Aliongeza kuwa kuogelea pia kunamsaidia kukutana na watu wa rika lake, ingawa alisikitika kuwa washiriki wa kitengo cha waogeleaji waliozidi miaka 70 walikuwa wachache mno.

“Naomba watu waogelee, hasa wanawake ili waweze kumaliza matatizo ya mgongo,” akashauri.

Wakati huo huo, Rais wa Shirikisho la Mashindano ya Uogeleaji Nchini (Kenya Aquatics), Maureen Awiti, alifichua kuwa wanapanga kuandaa mashindano ya kitaifa ya Masters hapo Machi 2025 katika bwawa la kimataifa la Kasarani, Nairobi,  kuchagua timu ya taifa.

“Naomba Wakenya wajitokeze Kasarani ili tuchague timu itakayoshiriki Mashindano ya Kuogelea ya Dunia ya Masters nchini Singapore,” akasema Awiti.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*