Yahofiwa ndoa za utotoni zitaendelea kushuhudiwa hadi 2092 – Taifa Leo


HUKU Kenya ikipambana kukomesha ndoa za utotoni, ripoti ya kushtua ya Umoja wa Mataifa (UN) inatoa hali mbaya: kwa kiwango cha sasa, desturi hiyo itaendelea hadi 2092.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka huu ya UN kuhusu shabaha za Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDRs) ya Umoja wa Mataifa, watoto wachanga wa siku hizi watakuwa babu na nyanya kabla ya ndoa za utotoni kuangamizwa.

Takwimu zinaonyesha tofauti kubwa kati ya wakazi wa mijini na wa vijijini. Ripoti inaonyesha nchini Kenya ndoa za utotoni katika maeneo ya mijini ni asilimia 15, huku maeneo ya mashambani yakirekodi asilimia 20.

Serikali inatambua kwamba ndoa za utotoni huchochewa na umaskini, ukosefu wa elimu, thamani ya chini ya kijamii na kiuchumi inayowekwa kwa wasichana, na ushawishi wa mila na desturi za kidini.

Hali hii inazidishwa na majanga ya asili, migogoro na milipuko ya magonjwa. Serikali inaeleza kuwa inajitahidi kukomesha ndoa za utotoni kupitia sheria kama vile Sheria ya Watoto (2022), ambayo inaharamisha kuoa mtoto, na Sheria ya Ndoa (2014), ambayo inaruhusu ndoa kwa watu wenye umri wa miaka 18 na kuendelea.

Wasichana waliopata hifadhi katika Shule ya Chemolingot Day/Boarding Primary School eneo la Tiaty, Kaunti ya Baringo, mnamo 2022. PICHA | JARED NYATAYA

Lakini ukweli halisi wa mambo mashinani unaelezea hadithi tofauti. Umaskini, ukosefu wa elimu, kukosekana kwa miundombinu ifaayo, majanga ya kiasili, na thamani ndogo ya kijamii na kiuchumi inayowekwa kwa wasichana, vyote vinachangia kuendeleza desturi ya kuwaoza wasichana wadogo.

Hili lilikuwa wazi katika mahojiano kwa njia ya simu, kupitia mfasiri, na msichana mchanga ambaye aliolewa akiwa mtoto wakati wa mvua. Lokedo* aliolewa katika kijiji cha kwao, Nanam, Turkana Magharibi, Kaunti ya Turkana.

Wakati huo, kijiji hicho kilikuwa kimekatwa kutoka maeneo mengine, huku barabara zikiwa hazipitiki kwa kufurika maji na mito ya msimu iliyojaa maji chafu.

“Mama yangu aliniamsha asubuhi. Aliniambia ni siku ya harusi yangu. Bwana harusi alikuwa tayari amefika,” Lokedo alisema.

Lokedo hakuwahi kwenda shule na hazungumzi wala kuelewa Kiswahili. Pia hakukumbuka aliolewa lini au alikuwa na umri gani. Alichokumbuka ni kwamba hakuwa na matiti.

“Nilitaka kukimbilia mahali popote mbali sana, lakini ningewezaje kufanya hivyo mafuriko yakiwa kila mahali?” alisema na kuongeza kuwa “nililia mpaka nikaishiwa nguvu za kulia tena. Kwa hiyo, nilikubali tu hatima yangu.”

Lokedo anasema “mume” wake alikuwa kijana lakini alifariki kabla ya kujifungua binti yake wa kwanza. Baadaye alirithiwa na sasa ana watoto wengine wawili wasichana.

Wakati huo, shirika la kutetea haki za binadamu lilikuwa limeshirikiana na serikali kuwawezesha wenyeji kiuchumi na kuwashauri dhidi ya kuwaoza binti zao.

Wasichana waliokimbia ndoa za mapema wakiwa katika kituo cha Cana Girls Rescue Home in Nginyang’, Kaunti ya Baringo, mnamo 2018. PICHA | JARED NYATAYA

“Tumewafunza 280 kati yao katika Kaunti Ndogo ya Turkana Magharibi, na kila mmoja wao anatarajiwa kufikia wengine 20. Na kila mmoja wa 20 anapaswa kufanya vivyo hivyo,” Bw Walter Mounde, afisa wa jinsia na ushirikishaji wa kijamii katika Shirika la Misaada la ADRA Kenya), aliambia Taifa Leo.

Alisema waliwafundisha wasichana na wanawake vijana wenye umri wa miaka 15-24, ambao baadhi yao walilazimishwa kuolewa kabla ya kufikisha miaka 18.

Bw Mounde alisema wale walio na uzoefu hueleza uchungu na dhiki zao kwa jamii ili waelewe ni kwa nini ni muhimu kuacha kutafutia wachumba watoto wao kinyume na matakwa yao.

“Hatuwaelekezi tu kuwapa taarifa za kukomesha ndoa za utotoni, tunatambua kuwa uhuru wa kifedha pia ni jambo la msingi. Hivyo tumewasaidia kuanzisha vyama vya kuweka na kukopa vijijini ili waanzishe biashara za kuwajengea uwezo wa kustahimili maisha yao na kuwapeleka watoto wao shule,” akaeleza.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*